Saumu Mwalimu
UNAPOTAJA historia ya nchi Tanzania, ni dhahiri 
kwamba hutaacha kutaja majina ya wapigania uhuru na viongozi mbalimbali 
walioiongoza tangu enzi za ukoloni, hadi kupata uhuru.
Hata hivyo,
 katika kila historia ya taifa lolote iliyojengwa, kuna watu 
waliofanikisha historia hiyo, lakini kwa sababu moja au nyingine, 
michango ya baadhi yao imesahaulika na pengine kutotajwa kabisa kwenye 
historia hizo.
Wengi wa Watanzania tunafahamu kuwa jina la nchi 
yetu Tanzania, limetokana na majina ya nchi mbili zilizoungana na kuwa 
moja ambazo ni Tanganyika na Zanzibar. Hivi ndivyo tulivyofundishwa 
shuleni.
Wengine wanaamini kuwa Rais wa kwanza na muasisi wa taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyebuni jina la Tanzania.
Lakini
 ukweli ni kwamba, jina la Tanzania lilibuniwa na mmoja wa wananchi 
walioshiriki mchakato wa kutafuta jina la nchi hii, baadaya muungano wa 
Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964.
Mohammed Iqbal Dar ndiye 
aliyebuni jina la Tanzania, wakati huo akiwa na umri wa miaka 18 akiwa 
mwanafunzi wa Shule ya Sekondari  Mzumbe.
Ilikuwaje? “Nilikuwa
 maktaba najisomea, nilishika gazeti la Daily News, wakati huo likiitwa 
The Standard, ndipo nikaona tangazo hilo,” anaeleza Dar alivyopata 
hamasa na kuongeza:
“Siku hiyo hiyo, nikafanya majaribio ya kutafuta 
jina bila hata ya kuishirikisha familia yangu. Nilichuka karatasi na 
kalamu, lakini kabla sijaanza kufanya chochote, nilimwomba Mungu 
aniwezeshe kwa maana naamini Mungu, ndiye kila kitu wakati wa kufanya 
jambo lolote.”
“Kwa hiyo kwenye ile karatasi nikaandika Tanganyika
 na Zanzibar kisha, nikaandika majina yangu mawili;  Iqbal na Ahmadiya,”
 anasema Dar na kufafanua kuwa Iqbal ni jina lake na jina la ubini na  
Ahmadiyya ndiyo dhehebu lake.
Kupata jina Tanzania
Akisimulia alivyopata jina Tanzania, anasema kuwa ilimchukua dakika tano tu kufikiria na kulipata jina hilo.
“Nilichukua
 Tan kutoka kwenye Tanganyika na kuongeza Zan kutoka kwenye Zanzibar na 
kupata Tanzan, niliona halitimii vizuri,”anasimulia Dar.
Anabainisha
 kuwa baadaye alifikiria na kugundua kuwa majina mengi ya nchi za Afrika
 yanaishia na IA mfano akitoa mfano wa Ethiopia, Gambia, Tunisia, 
Nigeria, Algeria, Somalia, Zambia, Namibia na kwamba baada ya kubaini 
hilo aliamua kuongezea herufi hizo mbili na kupata jina Tanzania.
“NIlituma maombi yangu katika shindano hilo, bila kumwambia mtu yeyote nyumbani,” anasema Dar. 
Baada
 ya muda mfupi baba yake, mzee Tufail Ahmad Dar, alipokea barua kutoka 
Wizara ya Habari na Utalii (wakati huo), ambapo ndani yake kulikuwa na 
ujumbe wa pongezi ya kwamba kijana wake ameshinda katika shindano hilo.
“Wakati
 naandika, sikuwa na matumaini kama nitashinda kwa kuwa shindano hilo 
lilikua wazi kwa watu mbalimbali, hivyo sikuwa na tarajio lolote kama 
ningeshinda,
“Jioni wakati narudi nyumbani, baba mzazi 
alinifungulia mlango wakati si kawaida yake kwani mama ndiye alikuwa 
akinifungulia siku zote, hapo nikajua kuna kitu hakipo sawa. Lakini, 
nilikaribishwa na tabasamu la baba, pamoja na pongezi nyingi, nilifurahi
 sana,” anaeleza.
TuzoDar anasema kuwa kwa ushindi huo, alitunukiwa ngao pamoja na fedha taslimu Sh200 kama zawadi ya ubunifu wake.
Pamoja
 na kuibuka mshindi wa ubunifu huo na hadi leo jina la Tanzania 
alilolibuni yeye linaendelea kutumika, lakini Dar anadai kuwa mchango 
wake huo kwa taifa ni kama hautambuliwi na Serikali imemsahau katika 
kuandika historia ya taifa la Tanzania.
“Sijui kwa nini 
sitambuliwi tangu wakati huo? Hakuna chochote kinachoelezea uhusika 
wangu katika kupata jina la Tanzania na ukiwauliza watu, wengi 
watakwambia ilikuwa ni Nyerere aliyeleta jina Tanzania, hii inaumiza,” 
anasema akilalamika.
Tanzania ya sasaBaada ya
 miaka 13 tangu kufariki kwa Nyerere,  Dar anasema kuwa Tanzania 
haimtendei haki mwasisi huyo wa Taifa, ambalo ni kisiwa cha amani.
“Ni
 kama imepita miaka mingi sana tangu kifo chake. Watanzania wamesahau 
kila kitu alichokiota Mwalimu Nyerere. Nakumbuka moja ya vita kubwa 
aliyopigana ni dhidi ya rushwa, yeye aliichuki rushwa lakini kwa sasa, 
rushwa imekua kama ndiyo tafsiri ya maisha ya Tanzania. Hakuna kitu 
kinachoweza kufanyika kwa urahisi hata kama ni haki ya mtu, bila kutoa 
rushwa,” anasema.
Anaongeza kuwa: “Mwalimu Nyerere alikua ni 
rafiki ya baba yangu na walikua wakionana na kuongea, nakumbuka siku 
moja kulikuwa na sherehe nyumbani na kwa kuwa tulikuwa watoto, 
nilimhudumia chai Mwalimu.
“Nakumbuka Mwalimu aliwahi kumuuliza 
baba yangu; Lini Malaria itaisha nchini hii? Baba alimjibu kuwa, kamwe 
malaria haitaisha ikiwa hakutakuwa na kujitolea kwa kila mmoja wetu, 
bila kumtegea mwengine,” anasema.
Katika kumbukumbu ya kifo cha 
Baba wa Taifa, Dar anaishauri Tanzania iendeleze misingi ya maisha 
ambayo Hayati Mwalimu Nyerere aliisimmamia, ikiwamo umoja na 
mashikamano, ili kuondoa tofauti kubwa kati ya maskini na matajiri.
“Tunaona
 namna ambavyo matajiri wanendelea kuwa tajiri zaidi, wakati maskini 
wanazidi kudidimia. Kama kungekuwa na ushirikiano kati ya watu hawa 
wawili, tofauti kati yao ingekuwa ndogo au isingekuepo kabisa,” 
anaeleza.
Anashauri pia kuwepo na sanamu za utambulisho ya Baba wa
 Taifa kila mahali, ili kulienzi jina lake liishi milele. “Kwa 
ninavyomjua Mwalimu natamani jina lake liishi milele na litangazwe 
lijulikane dunia nzima,”anasema.
Mohammed Iqbal Dar aliazaliwa mwaka 1944 jijini Tanga, ni mtoto wa tatu kati ya watoto saba wa Tufail Ahmad Dar.
Dar
 ni baba wa mtoto mmoja, ambapo kwa zaidi ya miaka 40 sasa amekuwa 
akiishi nchini Uingereza alikoenda kwa ajili ya kusoma kabla ya kuwa 
raia wa nchi hiyo.
Mbunifu huyo wa jina la Tanzania ni Mhandisi wa
 Masuala ya Redio, kazi anayoifanya nchini Uingereza, akieleza kuwa 
katika kuienzi nchi yake, nyumba yake iliyopo mjini Birmingham, ameipa 
jina la Dar es Salaam, ikiwakilisha ubini wake, pamoja na Jiji la Dar es
 Salaam.