Hussein Semdoe, Kilindi 
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya 
Wilaya ya Kilindi ,mkoani Tanga, limewafuta kazi watumishi wawili  kati 
ya 15 wa halmashauri hiyo waliokuwa wakikambiliwa na utata wa 
ubadhirifu.
Watumishi wengine watatu kati ya hao wamevuliwa 
madaraka yao kwa madai ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali 
yaliyoisababishia hasara Serikali. 
Watumishi hao waliochukuliwa 
hatua hizo ni miongoni mwa wafanyakazi 15, wa halmashauri hiyo, 
waliokuwa wakihusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma. 
Madiwani
 hao walifikia uamuzi huo mwishoni mwa wiki katika kikao cha halmashauri
 hiyo maarufu kwa jina la ‘Waseuta Nougone’, kilichofanyika chini ya 
Mwenyekiti wake Mussa Semdoe na Mkurugenzi Mtendaji Daudi Mayeji.
Awali,
 katika mkutano huo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi,
 Pascal Lefi, aliwasilisha taarifa ya kamati ya uchunguzi wa watumishi 
waliokuwa na tuhuma mbalimbali kwa niaba ya Mkurugenzi, na kutaja majina
 ya watumishi 10 waliokuwa wamefunguliwa mashtaka ya nidhamu. 
“Halmashauri
 ya Wilaya ya Kilindi ilikumbwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za 
umma, hali iliyofanya uongozi  kuomba kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa 
Serikali kuja kufanya ukaguzi maalumu, kwa hesabu za mwaka 2008, 2009 na
 2010. Baada ya kukamilika ukaguzi huo jumla ya watumishi 15 
walihusishwa na tuhuma hizo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na 
kuongeza. 
“Matokeo ya ukaguzi huo yamefanya watumishi watano 
wasimamishwe kazi na kupelekwa katika vyombo vya dola ama sheria, 
wengine wanne walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi na watumishi wengine
 sita waliendelea na kazi huku tuhuma zikiendelea,” alisema Mkurugenzi 
huyo. 
Mayeji aliwataja watumishi waliofutwa kazi kuwa ni Robert 
Kwayi, aliyekuwa ni mhasibu, ambaye ametiwa hatiani na kamati hiyo, 
kutokana na uzembe uliosababisha halmashauri hiyo kupata hasara ya Sh 80
 milioni, na Edward Kapwapwa, ambaye ni Afisa Kilimo Msaidizi, 
aliyetimuliwa kazi kutokana na utoro kazini. 
Aliwataja maofisa 
waliovuliwa madaraka, kuwa ni pamoja na, Fredrick Kiango, aliyekuwa 
Afisa Kilimo na mifugo wa Wilaya ya Kilindi, ambaye amekutwa na hatia ya
 Uzembe uliosababisha wilaya hiyo kupata hasara ya Sh 80 milioni, kwa 
kushindwa kushauri vizuri katika ununuzi wa Power Tiller zilizokuwa na 
upungufu.