Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Rais Kikwete alisema hayo juzi katika hotuba yake ya ambayo
huisoma kila mwishoni mwa mwezi, kauli ambayo imekuja wakati kukiwa na
malalamiko kwamba Serikali imekuwa ikifumbia macho matukio ya uhalifu
wenye sura ya uhasama wa kidini.
“Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za
Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu
nyinginezo,” aliongeza Rais Kikwete.
Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisema
nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo na kwamba amekuwa akipendelea
kushiriki zaidi katika shughuli za Kikristo kuliko za Waislamu.
“Naambiwa kuwa niko mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko ya masheikh wanapofariki.
“Kuna misikiti mitatu ya Jijini Dar es Salaam ambayo iliwahi kunisomea itikafu ili nife kwa sababu za kubagua dini yao.
“Katika
itikafu hiyo waliwajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,”
alieleza Kikwete.
“Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo,” alisema.
Alifafanua pale ambapo hakushiriki mazishi ya
sheikh au askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine
ambazo ni lazima zifanywe na yeye au taarifa ilikuwa ya muda mfupi.
“Waislamu
desturi yetu ni kuzika mara mtu anapofariki, hicho ni kikwazo kwangu
kushiriki mazishi ya masheikh hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa
sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda
pengine siyo nyepesi,” alisema Kikwete.
Alisema pia Waislamu wanadai kuwa kitabu chao
kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa
moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yoyote ya
maana. Alisema imefika mahali viongozi na waumini wa dini hizo kubwa
mbili kama hawatakubali kubadili mwelekeo wa sasa basi tunakoelekea ni
kubaya
“Nchi yetu tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu
na Wakristo kuishi pamoja kama ndugu itatoweka. Tanzania itaacha kuwa
kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata
vita ya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Kikwete.
Alisema Serikali haifurahishwi na kitendo cha
mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya
Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo ambao wamekamatwa na
kufunguliwa mashtaka katika matukio tofauti.
“Vyombo vya usalama
vinatambua wajibu wao na kama havitimizi wajibu wao huo utakuwa ulegevu
wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali,” alisema
Kikwete.
Aliongeza; “Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha
wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya usalama kuacha ajizi katika
kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.”
Kikwete alisema kuuawa kwa viongozi wa dini na
kuchomwa makanisa kusichukuliwe kama Serikali yake imeshindwa kulinda
usalama wa raia wake.
“Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji
ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa
mengi hapa nchini,” alisema Rais Kikwete.
Ajali ya Jengo la ghorofa lililoanguka
Kikwete
alisema sheria zitafuata mkondo kwa waliosababisha kuanguka kwa jengo
hilo baada ya uchunguzi unaofanywa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi.
Alisema
watakaobainika kuhusika watatakiwa kufikishwa mahakamani ikiwa ni
pamoja na kufutiwa leseni zao za kuendesha shughuli za ujenzi.
Alitaka
mikoa yote nchini kujifunza katika ajali hiyo kwa kufuata kanuni za
ujenzi ili kuondokana na maafa yanayoweza kujitokeza.