hii picha sio halisi
Mwanafunzi wa kidato cha pili katika 
Sekondari ya Kiparang’anda wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Ismail 
Mohamed (15), amefariki baada ya kuchomwa kisu na kijana mwenzake, 
Ramadhani Mkamba (19), wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya.
Tukio hilo lilitokea saa 5:20, usiku wa mkesha wa 
mwaka katika eneo la CCM II Mbagala Kiburugwa, maarufu kama Magenge 20, 
tukio ambalo chanzo chake ni Sh200.
Akisimulia tukio hilo, katika Kituo cha Polisi 
Mbagala Kizuiani (Maturubai), Mjomba wa Marehemu, Nurdin Mohamed 
aliliambia Mwananchi, lililoambatana na kikosi cha doria cha Polisi 
Temeke kuwa mtuhumiwa alimchoma kisu Mohamed kifuani, baada ya kumnyima 
Sh200.
Alisema Mohamed ambaye alikuwa amefika nyumbani 
kwake hapo kwa ajili ya likizo, alikutana na mtuhumiwa huyo wakati 
akitoka magengeni ambapo walikuwa wakifanya biashara ya kuuza samaki.
Alisema mtuhumiwa alimwomba Mohamed Sh200 lakini 
alisema hana, mtuhumiwa alimpora simu yenye thamani ya Sh20,000, halafu 
akamchoma kisu kifuani kisha akakimbia.
Alisema baada ya mtuhumiwa kumchoma kisu Mohamed 
na kukimbia, yeye alimchukua majeruhi na kumpeleka katika Kituo cha 
Polisi Mbagala Kizuiani, ili aweze kupata fomu namba 3 ya Polisi kwa 
ajili ya matibabu, lakini wakati taratibu za kupata fomu hiyo 
zikiendelea, majeruhi alifariki.
Mtuhumiwa alifuatiliwa na kikosi cha doria ambacho kilifanikiwa kumtia mbaroni na kumfikisha kituoni hapo.
Katika tukio lingine, dereva teksi mmoja 
aliyefahamika kwa jina la Daniel Magori anayekadiriwa kuwa na umri wa 
miaka 35 na 40, amenusurika kifo baada ya kuchomwa kisu tumboni na 
majambazi na kisha kumpora gari.
Tukio hilo lilitokea kati ya saa 6:15 na saa 6:30, usiku wa kuamkia Mwaka Mpya , katika eneo la Imasko wilayani Temeke.
Baadhi ya wananchi walishauri Watanzania kuwa makini hasa katika nyakati za sikukuu ili kuepuka hali kama hizo.
 
 
No comments:
Post a Comment