
 wanafunzi wa shule ya msingi wakiwa darasani,hii ndio tofauti kubwa kati ya shule yenye kutoa maarifa na ujuzi na 
shule yenye kutoa vyeti na sifa za kumuwezesha mtu kupata kazi.
MATOKEO mazuri au mabaya  ya elimu kwa mtu,  huonekana katika 
namna anavyotenda mambo na dhamira yake ya kutenda,  na wala hayatokani 
na alichojifunza, namna alivojifunza na sababu ya kujifunza.
Hiyo ndio tofauti kubwa kati ya shule yenye kutoa 
maarifa na ujuzi na shule yenye kutoa vyeti na sifa za kumuwezesha mtu 
kupata kazi.
Watu wengine wanapozungumzia elimu wanafikiri 
kuhusu utaratibu mzima wa kujifunza wenye lengo la kumpatia mtu ujuzi na
 maarifa na kumudu vyema kile alichojifunza.
Ujuzi na maaarifa ndio hasa lengo na upatikanaji 
wake  unaotarajiwa utumike katika kupambana na changamoto na hata kuibua
 na kuleta maarifa mengine zaidi.
Kuna watu wengine wanapozungumzia elimu,  wanafikiria umiliki wa cheti kinachoonyesha una ujuzi fulani.
Elimu ya aina hii sio kwa ajili ya kutumika katika
 maisha wala kutafuta maarifa mengine,  bali ni kwa ajili ya mtu 
kukariri anachojifunza na  kuyatoa yale maarifa yaliyokaririwa katika 
mitihani ili apate cheti kizuri kitakachowezesha kupata kazi yenye 
kipato kizuri.
Kimsingi,  cheti kazi yake ni kumpatia mtu kazi. Cheti ndio ‘pasipoti’ ya kwenda katika nchi ya kipato.
Watanzania wengi kama sio wote,  tumeangukia 
katika kundi hili. Wengi wetu tunataka pasipoti ya kwenda katika ‘nchi’ 
ya kipato cha kuajiriwa, tunataka vyeti!
Katika mfumo wetu wa elimu 
mpaka sasa ufaulu wa mtihani ndio unaosema fulani apangiwe shule gani, 
apangiwe kozi gani  chuoni, apate kiasi gani kwenye mikopo ya elimu ya 
juu na apangiwe kazi gani na alipwe kiasi gani.
Sasa kuna vita kati yetu, kila mmoja anataka mwanawe, yeye mwenyewe au ndugu yake  afaulu ili afike katika nchi ya ahadi.
Mbinu mbalimbali zinatumika  kufanikisha lengo 
hili, vita haina macho! Mbinu kuu ikiwa matumizi ya pesa. Kusoma shule 
nzuri na ghali, kulipia twisheni, walimu bora, kununua vitabu na 
mwishowe hata kununua mitihani.
Mchakamchaka  huu wa kutaka kufaulu kisha kupata 
vyeti,  unawaacha nyuma watu wa kipato cha chini kwani hawawezi kumudu 
kununua mitihani, au kusoma twisheni  za gharama.
Wenye nacho wananeemeka na mtindo huu. Mwelekeo unaonyesha masikini  wataachwa kwa kiasi kikubwa na wenye uwezo.
Mwanzo wa kujenga matabaka mawili kupitia elimu bila kificho  unaonekana.