
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati 
na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo cha bidhaa za mafuta 
kinayoonyesha kuwa petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeshuka kuanzia 
leo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna 
Masebu imesema bei hizo zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la
 Desemba 5, mwaka jana.
 
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa petroli, 
dizeli na mafuta ya taa, zimepungua kwa viwango vifuatavyo: petroli 
Sh126 kwa lita sawa na asilimia 5.96; dizeli Sh32 kwa lita sawa na 
asilimia 1.60 na mafuta ya taa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.50,” 
imeeleza taarifa hiyo.
Kwa punguzo hilo, bei ya rejareja ya petroli 
katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh1,993, dizeli Sh1,967 na 
mafuta ya taa Sh1,973. Arusha petroli ni Sh2,077, dizeli Sh2,051 na 
mafuta ya taa Sh2,057.
Katika jiji la Mbeya petroli itauzwa kwa Sh2,099, 
dizeli Sh2,074 na mafuta ya taa Sh2,079 na jijini Mwanza, petroli 
itauzwa kwa Sh2,142, dizeli Sh2,117 na mafuta ya taa Sh2,122.
Taarifa
 imefafanua kuwa mbali na kupungua bei hiyo katika uuzaji wa rejareja, 
bei pia imepungua kwa katika uuzaji wa jumla ikilinganishwa na matoleo 
mawili yaliyopita.
“Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili
 zimepungua kama ifuatavyo: petroli kwa Sh126.10 kwa lita sawa na 
asilimia 6.17; dizeli kwa Sh32.48 kwa lita sawa na asilimia 1.69 na 
mafuta ya taa kwa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.6,” alisema.
Mkurugenzi huyo amesema katika taarifa hiyo kuwa 
mabadiliko hayo ya bei, yametokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika 
soko la dunia na kuimarika kidogo kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania 
dhidi ya Dola ya Marekani.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli, zitaendelea kupangwa na soko.
“Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa 
taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la 
kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za 
mafuta,” alisema Masebu.
Hata hivyo, Masebu alisema pamoja na mpango huo wa
 Ewura kuweka bei ya kikomo, kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa 
hizo kwa bei ya ushindani, ilimradi ziwe chini ya bei hiyo kikomo.
Alivitaka vituo vya mafuta kuchapisha bei hizo 
mpya katika mabango yanayoonekana bayana na kuonyesha bei ya mafuta, 
punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo 
husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja 
wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza 
mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza 
mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na 
adhabu itatolewa kwa kituo husika,” alisema.
Masebu aliwashauri wanunuzi kuchukua stakabadhi ya
 malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta 
yaliyonunuliwa na bei kwa lita ili itumike baadaye kama kidhibiti endapo
 kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko ya 
kikomo au yenye kiwango cha ubora kisichofaa.