
MWANAFUNZI  wa kidato  cha tatu katika shule ya Sekondari ya 
Tongoni nje kidogo ya jiji la  Tanga,  (jina tunalihifadhi) amekutwa 
amekufa ndani ya nyumba ya kulala wageni alikopelekwa kutolewa mimba 
bila mafanikio.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana na 
kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe
 mwanafunzi huyo alikutwa amekufa juzi katika nyumba ya kulala wageni 
iliyopo barabara ya 21 jijini Tanga.
                
              
Mmoja wa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni 
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe alisema kwamba mwanafunzi huyo 
aliingia saa 4.00 asubuhi siku ya tukio akiwa ameambatana na kijana 
mmoja wakakodi chumba.
                
              
“Baadaye alikuja mwanaume mmoja wa makamo ambaye 
alituuliza kama wameingia mwanafunzi huyo na mwenzake, tulipomwonyesha 
chumba  walichoingia naye akakodi chumba cha jirani ndipo tukaona wote 
wakijifungia kwenye chumba kimoja,” alisema mhudumu.
                
              
Mhudumu huyo alisema baada ya muda wa saa moja, 
mvulana na mzee huyo wakaaga kwamba wanatoka huku wakisema kwamba 
msichana amebaki chumbani akiwa amepumzika. Akithibitisha habari hizi, 
Kamanda Massawe alisema taarifa ya tukio hilo ilitolewa na mhudumu wa 
nyumba hiyo ya kulala wageni katika Kituo cha Polisi cha Chumbageni 
Jijini Tanga.
                
              
“Tatizo ni kwamba nyumba hii ya wageni wahudumu 
wake hawakuwapa wageni hao daftari ili waorodheshe majina yao hivyo 
inakuwa vigumu  kuwafahamu,” alisema Kamanda Massawe na kufafanua kuwa 
alifariki akitolewa mimba ya mwezi mmoja.
                
              
Kamanda Massawe alisema mpaka sasa hakuna mtu 
aliyekamatwa na kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini 
waliohusika na kifo hicho.Raisa Said, Tanga
 
 
No comments:
Post a Comment