Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana.
Na: Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
Serikali imeombwa kuongeza kiasi 
cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na 
Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi 
milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo 
ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na 
baadhi ya  vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na 
halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na 
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  
alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza 
kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za 
mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na 
kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za 
shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali 
kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji 
cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne 
kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na
 kulipa wasaidizi wanaohudumia  shamba lake la migimba na kahawa  
ambalo  ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni
 na Nyakibimbili na kwenda  kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na 
changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka
 na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa 
kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia 
jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na  
magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa  kikundi cha 
Msifuni  Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na
 laki tano  kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba  alisema kuwa kikundi
 chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa  samaki  na walianza na 
bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha
 kuwa   kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni 
kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha 
na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa 
samaki  ikiwa ni pamoja na kuibiwa  na kuharibiwa kwa mabwawa hasa 
nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema
 Joel.
Kwa upande wake waziri Dk. 
Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na 
kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo ambalo litawafanya waweze 
kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na halmashauri ya 
wilaya na hivyo kuweza   kujishughulisha na kazi  za upandaji wa miti, 
kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana  ni
 lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu,  kufanya kazi si 
lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera 
kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi 
wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na mkiiuza 
mtapata fedha nahivyo  kujikwamua kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya 
ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa wizara yake inavituo vya 
kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika ambao ni vijana watakuwa
  tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, 
stadi za maisha watayapata  na yatawasaidia katika maisha yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa 
mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana  
vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha 
hizo zimewasaidiaje  vijana kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba
 alilitembelea shamba la mfano la kahawa na migomba, kikundi cha 
burudani cha  Rugazi na  shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.
 
 
No comments:
Post a Comment