Thursday, October 4, 2012

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MTIHANI WA KIDATO CHA NNE NA MTIHANI WA MAARIFA OKTOBA, 2012

Ndugu Wananchi,
Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 utafanyika nchini kote kuanzia tarehe 08, hadi tarehe 25 Oktoba, 2012. Jumla ya watahiniwa walioandikishwa kufanya mtihani ni 481,414 wakiwemo wavulana 263,202 sawa na asilimia 54.67 na wasichana 218,212 sawa na asilimia 45.33. Idadi hiyo ya watahiniwa wote walioandikishwa mwaka 2012 ni ongezeko la watahiniwa 31,090 sawa na asilimia 6.90 ikilinganishwa na watahiniwa 450,324 walioandikishwa kufanya mtihani huo mwaka 2011.  Watahiniwa wote walioandikishwa kufanya mtihani mwaka 2012 wamegawanyika katika makundi matatu kama ifuatavyo:-
·         Watahiniwa wa shule (School Candidates) ni 412,594 wakiwemo wavulana 228,991 sawa na asilimia 55.50 na wasichana 183,603 sawa na asilimia 44.50.  Watahiniwa hao wa shule wa mwaka 2012 ni ongezeko la watahiniwa 63,204 sawa na asilimia 18.09 ikilinganishwa na watahiniwa wa shule  349,390 wa mwaka 2011.
·         Watahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidates) ni 68,820 wakiwemo wanaume 34,211 sawa na asilimia 49.71 na wanawake 34,609 sawa na asilimia 50.29. Watahiniwa wa Kujitegenea walioandikishwa mwaka 2012 ni pungufu ya Watahiniwa 32,114 sawa na upungufu wa asilimia 31.82 ikilinganishwa na watahiniwa 100,934 walioondikishwa mwaka 2011.
·         Mtihani wa Maarifa (Qualifying Test) utafanyika tarehe 16 Oktoba, 2012. Jumla ya watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa walioandikishwa ni 21,314 wakiwemo wanaume 8,174 sawa na asilimia 38.35  na wanawake 13,140 sawa na asilimia 61.65. Watahiniwa wa Maarifa walioandikishwa mwaka 2012 ni pungufu ya watahiniwa 8,133 sawa na upungufu wa asilimia 27.62 ikilinganishwa na watahiniwa 29,447 walioandikishwa mwaka 2011. 
Watahiniwa wote wameandikishwa katika shule/vituo vilivyotawanyika katika Mikoa mbalimbali nchini kama ifuatavyo:-  Jumla ya shule 4,155 zina Watahiniwa wa Shule (School Candidates).   Watahiniwa wa Kujitegemea (Private candidates) wameandikishwa katika vituo 902; na Watahiniwa wa Maarifa (Qualifying Test) wameandikishwa katika vituo 616.
Ndugu wananchi,
Hadi sasa maandalizi na usafirishaji wa mitihani hiyo hadi ngazi ya mikoa yamekamilika. Aidha, mikoa inaendelea na taratibu za kuhakikisha kuwa kila kituo kinapata mitihani yake kwa muda uliopangwa kwa kuzingatia taratibu na maelekezo ya Baraza la Mitihani la Tanzania.
Ndugu Wananchi,
Kuhusu usalama wa mitihani, hadi sasa mitihani yote ipo salama, na hakuna mtihani uliyovuja katika ngazi yoyote kuanzia Baraza la Mitihani, Mikoa na Halmashauri. Ninatoa pongezi kwa Baraza la Mitihani kwa kuandaa mitihani hiyo na kuisafirisha kwa usalama hadi ngazi ya mkoa. 
Ninatoa wito kwa Kamati za Mitihani za mikoa yote kuhakikisha kuwa taratibu zote za utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa mitihani hiyo zinazingatiwa. Ni matumaini yangu kuwa ufuatiliaji na ukaguzi wa usalama wa kila kituo umefanyika na hatua za kurekebisha mapungufu kama yapo zimefanyika.
Ndugu Wananchi, 
Mtihani wa Kidato cha Nne ni muhimu sana kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla, kwani hutumika katika uchaguzi wa watahiniwa wanajiounga na masomo ya Kidato cha Tano na Vyuo mbalimbali.  Aidha, ili kuweza kujiunga na soko la ajira katika taasisi za umma au sekta binafsi ni lazima mhusika awe na cheti cha Kidato cha Nne.  Hivyo mtihani wa Kidato cha Nne ni muhimu sana kwa maisha ya watahiniwa na wananchi kwa ujumla.
Ndugu wananchi
Ufanisi wa zoezi muhimu kama la mitihani unahitaji ushirikiano wa wadau wote. Ninatoa wito kwa wananchi wote, wakiwemo Viongozi, walimu, Wazazi, Jamii na  Wasimamizi wa mitihani kutoa ushirikiano wa kutosha na kuhakikisha kuwa mazingira yanakuwa ya amani na utulivu kipindi chote cha mitihani. Wakuu wote wa vituo vya mitihani hakikisheni kuwa mahitaji yote ya msingi kuhusu mitihani yanapatikana. 
Ndugu Wananchi,
Kutokana na muhimu wa mtihani wa Kidato cha Nne katika  kutoa mwelekeo wa  maisha ya watahiniwa kama ilivyofafanuliwa hapo juu, wapo baadhi ya watahiniwa na wasimamizi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani.  Watahiniwa wanaobainika kufanya udanganyifu katika mitihani wamekuwa wakifutiwa matokeo yao yote ya mitihani kwa mujibu wa Kanuni za Uendeshaji wa Mitihani ya Taifa. 
Ninachukua fursa hii kuwakumbusha watahiniwa kuwa, kila mtahiniwa afanye mitihani yake kwa kujitegemea bila udanganyifu. Wale wote watakaobainika kushiriki katika udanganyifu watachukuliwa hatua za kinidhamu. Nikirejea mtihani wa mwaka 2011, jumla ya watahiniwa wa Kidato cha Nne 3,303 walifutiwa matokeo yao kwa sababu ya kufanya udanganyifu. Aidha, walimu waliohusika walipewa adhabu mbalimbali ikiwemo onyo, karipio kali, kuvuliwa madaraka wakuu wa shule na wengine kushitakiwa TSD. Aidha, wenye shule waliothibitika kusababisha udanganyifu wameandikiwa barua ya kusudio la kuzuia kudahili wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kwa muda wa mwaka mmoja. 
Kuhusu watahiniwa waliofutiwa matokeo, baada ya kuomba msamaha wamepunguziwa adhabu, na wataruhusiwa kufanya mtihani mwaka 2013 kama watahiniwa wa kujitegemea baada ya kutumikia adhabu kwa muda wa miaka miwili. Ninatoa wito kwa walimu, viongozi na wazazi kuwaasa watahiniwa kuhusu swala la udanganyifu, kwani kwa mwaka huu adhabu haitapunguzwa. Ni matumaini yangu kuwa watahiniwa wote watazingatia taratibu zote za mitihani bila kujiingiza katika udanganyifu. Serikali haitasita kuchukua hatua kama ilivyokuwa mwaka 2012.
Ndugu Wananchi,
Ninarudia kutoa wito kuwa walimu, wasimamizi wa mtihani, Wakuu wa Shule, viongozi wote, na jamii kutoa ushirikiano na kuhakikisha kuwa mitihani inafanyika katika mazingira yenye usalama na amani.  Ninaomba wote tuungane kuwaombea Watahiniwa wetu Baraka za Mwenyezi Mungu na mafanikio katika mitihani yao.
Ndugu Wananchi,
Katika kuhitimisha taarifa yangu ninapenda pia kutoa ufafanuzi kuhusu Mtihani wa Taifa wa Kidato cha sita kwa wanafunzi walioko kidato hicho mwaka 2012/2013. Wanafunzi hao watafanya Mtihani wa Taifa mwezi Machi, 2013. Aidha, wanafunzi waliopo kidato cha 3 mwaka huu watafanya Mtihani wa Taifa wa kidato cha 4 mwezi Novemba 2013 kama ilivyoelekezwa na Kamishna wa Elimu kwenye Waraka wa Elimu Na. 5 wa Mwaka 2012 kuhusu Marekebisho ya Mihula ya Shule za Sekondari na Vyuo vya Ualimu.
  
PHILIPO A. MULUGO (Mb.)
NAIBU  WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI