Thursday, December 6, 2012

Familia Ya Sharo Yaibua Mazito

Mama Yake Hussein Sharo Millionea Akilia Kwa Uchungu


 Na: Burhani Yakub, Muheza
FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo Milionea) aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki
iliyopita imedai kuwa haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli.

Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu.


Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa  vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo liliwashangaza.
Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia, hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka.
Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha lakini hakuna damu zilizoonekana.


Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.


Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa  nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa zimeganda masikioni.


Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia  alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha pande zote.”



Mama yake alia kukosa mjukuu
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha awe akimkumbuka mwanaye huyo milele.
Akizungumza nyumbani kwake, katika Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo.


“Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia fedha za kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini kila mwisho wa mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi yangu na ndugu zake hapa nyumbani,” alisema mama huyo.
Alisema mwisho wa mwezi itakuwa ni alama ya kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni wakati ambao alikuwa akimtumia fedha za matumizi yake pamoja na
familia nzima.


Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele yangu,” alisema.


Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina.

darasa la kwanza na la pili waendelea kusomea kwenye darasa moja kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa unaoikabili Shule ya Msingi, yenye darasa la kwanza hadi la saba.

Hili ni darasa jipya lililojengwa sasa katika Shule ya Msingi Silabu iliyopo Wilaya ya Korogwe darasa hili linatumiwa na wanafunzi wa darasa la tatu



Mti huu kivuli chake ni ofisi ya walimu wa Shule ya Msingi Silabu iliyopo Wilaya ya Korogwe
 

Uchochoro huu ndio lililuwa darasa la tatu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Silabu iliyopo Wilaya ya Korogwe


Na Mwandishi wa Thehabari.com Korogwe WALIMU wa Shule ya Msingi Silabu Wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga bado wanatumia kivuli cha mti uliopo mbele ya shule hiyo kama ofisi ya walimu (staff room) kwa kukosa jengo la ofisi. 
Hiki ni kipindi cha miezi sita imepita sasa tangu mtandao wa Thehabari.com uripoti habari hii mapema mwezi Agosti 2012. Juzi mwandishi wa habari hizi alipita tena katika shule hiyo kuangalia juhudi za Serikali na wananchi kufanikisha ujenzi wa ofisi hiyo, lakini alishuhudia walimu wa shule hiyo wakiendelea kufanya shughuli zao chini ya mtimu.
 “…Hii ndiyo ofisi yetu bado,jengo ambalo tutalitumia kama ofisi halijajegwa shuleni hapa, hivyo tunatumia kivuli cha mti huu kama ofisi na wakati mwingine jua likizidi huamia pembezoni mwa kingo za darasa lenye kivuli,” alisema mmoja wa walimu ambaye alikutwa amekaa chini ya mti huku akiendelea na kazi. 
Hata hivyo mwalimu huyo hakuwa tayari kutaja jina lake kwa madai si msemaji wa shule hiyo, juhudi za kumpata Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Silabu, Mizeki Charahani ziligonga ukuta baada ya kuambiwa alikuwa nje ya shule kikazi. 
Awali mwezi Agosti mwandishi wa habari hizi aliripoti wanafunzi wa darasa la tatu katika Shule hiyo kusomea kwenye uchochoro unaotenganisha kati ya darasa moja na lingine kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Wanafunzi hao ambao darasa lao lilikuwa likihama kila muda kutengemea hali ya hewa (jua na mvua) kufuata kivuli walilazimika kusomea nje kwenye uchochoro ambao haujaezekwa kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa shuleni hapo. 
 Hata hivyo tayari limejengwa darasa moja ambalo kwa sasa linatumiwa na wanafunzi wa darasa la tatu, huku darasa la kwanza na la pili wakiendelea kusomea kwenye darasa moja kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa unaoikabili shule hiyo, yenye darasa la kwanza hadi la saba. 
*Imeandaliwa na www.thehabari.com