Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akiendesha ibada takatifu ya kubariki mafuta ya Krisma na kurudiwa kwa kiapo cha mapadri, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, jana. Picha na Emmanuel Herman.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini, Mwadhama Kardinali Polycarp
Pengo, amewataka mapadri wa Kanisa hilo kuwa kioo kwa matendo mema kwa
kila wanachokifanya kwa wengine.
Kardinali Pengo aliyasema hayo jana wakati wa misa
ya sherehe ya Sakramenti ya Upadri na kubariki mafuta ya Pasaka katika
Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph jijini humo.
Alisema ni lazima kuwa watimilifu wa kibinadamu
kwa kupitia njia ya sadaka, mateso na kifo hivyo kuwataka kuwafundisha
yaliyo mema na yenye kumpendeza Yesu Kristu.
“Ili kufikia ukamilifu hatuwezi kukwepa misalaba,
waumini mnatakiwa kutuombea ili kuweza kumwakilisha Yesu Kristu kwa
matendo yaliyo mema na ya kumpendeza,” alisema Kardinali Pengo. “Hivi
sasa shida na mahangaiko ya dunia ni mengi lazima kumwonyesha Yesu
ili aweze kutusadia na kushinda.
“Tukianza kuangalia chanzo cha matatizo na
mahangaiko yalivyo hivi sasa hatuwezi kufika na tutaangamia,” alisema
Kardinali Pengo.
Alisema njia nyingine zozote ambazo zinashabikia
kama anasa na ukatili haziwezi kufanikiwa, hivyo aliwataka Mapadri hao
kuwahubiria amani waumini.