Hussein Semdoe, Kilindi
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kilindi ,mkoani Tanga, limewafuta kazi watumishi wawili kati
ya 15 wa halmashauri hiyo waliokuwa wakikambiliwa na utata wa
ubadhirifu.
Watumishi wengine watatu kati ya hao wamevuliwa
madaraka yao kwa madai ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali
yaliyoisababishia hasara Serikali.
Watumishi hao waliochukuliwa
hatua hizo ni miongoni mwa wafanyakazi 15, wa halmashauri hiyo,
waliokuwa wakihusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Madiwani
hao walifikia uamuzi huo mwishoni mwa wiki katika kikao cha halmashauri
hiyo maarufu kwa jina la ‘Waseuta Nougone’, kilichofanyika chini ya
Mwenyekiti wake Mussa Semdoe na Mkurugenzi Mtendaji Daudi Mayeji.
Awali,
katika mkutano huo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi,
Pascal Lefi, aliwasilisha taarifa ya kamati ya uchunguzi wa watumishi
waliokuwa na tuhuma mbalimbali kwa niaba ya Mkurugenzi, na kutaja majina
ya watumishi 10 waliokuwa wamefunguliwa mashtaka ya nidhamu.
“Halmashauri
ya Wilaya ya Kilindi ilikumbwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za
umma, hali iliyofanya uongozi kuomba kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Serikali kuja kufanya ukaguzi maalumu, kwa hesabu za mwaka 2008, 2009 na
2010. Baada ya kukamilika ukaguzi huo jumla ya watumishi 15
walihusishwa na tuhuma hizo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na
kuongeza.
“Matokeo ya ukaguzi huo yamefanya watumishi watano
wasimamishwe kazi na kupelekwa katika vyombo vya dola ama sheria,
wengine wanne walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi na watumishi wengine
sita waliendelea na kazi huku tuhuma zikiendelea,” alisema Mkurugenzi
huyo.
Mayeji aliwataja watumishi waliofutwa kazi kuwa ni Robert
Kwayi, aliyekuwa ni mhasibu, ambaye ametiwa hatiani na kamati hiyo,
kutokana na uzembe uliosababisha halmashauri hiyo kupata hasara ya Sh 80
milioni, na Edward Kapwapwa, ambaye ni Afisa Kilimo Msaidizi,
aliyetimuliwa kazi kutokana na utoro kazini.
Aliwataja maofisa
waliovuliwa madaraka, kuwa ni pamoja na, Fredrick Kiango, aliyekuwa
Afisa Kilimo na mifugo wa Wilaya ya Kilindi, ambaye amekutwa na hatia ya
Uzembe uliosababisha wilaya hiyo kupata hasara ya Sh 80 milioni, kwa
kushindwa kushauri vizuri katika ununuzi wa Power Tiller zilizokuwa na
upungufu.