Wednesday, March 6, 2013

Ofisa elimu awavua madaraka walimu 50


https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjuCV9LyT-zhZFca_QDGQlRo9uMbdItAY9KdhW35_-VI-6yhGZ4njzDmAneWU72KyR_lzgFFEyWW3qZ8klrk9EzvZPLbdzqpmQZJzquBoB-526v3fi9lvIW4DNR3L5Rjq22qsvFmQy7AiU/s1600/HakiElimu2.JPG

Kilindi. Ofisa Elimu ya Msingi Wilaya ya Kilindi, Mkoa wa Tanga, Geofrey Abayo amewavua madaraka walimu wakuu 50 wa shule za msingi, lengo likiwa ni kusuka upya timu ya kuinua kiwango cha taaluma.
Abayo aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya matokeo ya darasa la saba mwaka jana wilayani hapa kuwa mabaya, baada ya asilimia 18 ya wanafunzi waliofanya mtihani ndiyo waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza.
Alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye mkutano na walimu wa shule za msingi na sekondari, uliofanyika katika kata tano za Kwediboma, Mabaranga, Negero, Kikunde na Songe.
Ofisa huyo akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman Liwowa  na Katibu Tawala Msaidizi Elimu Mkoa wa Tanga, Ramadhani Chomola walisema  walitarajia kupata matokeo hayo.
Alisema walitarajia watoto wengi kushindwa kutokana na kuongeza udhibiti katika usimamizi wa mitihani kitaifa kwa darasa la saba, kwa kuziba mianya inayotumiwa na baadhi ya walimu wasio waaminifu kuwapa majibu watahiniwa.
Abayo aliapa kuendelea kuwa mkali kwa walimu wanaowafanyia mitihani watoto ili wafaulu.
Mwalimu Ali Mganga wa Shule ya Msingi Kikunde, alipendekeza mitihani ya kitaifa ikishafanywa ipelekwe shuleni ili wanafunzi na walimu waweze kutambua walipojikwaa.
Hata hivyo, Mwalimu Mganga alitupia lawama kwa watungaji mitihani ya taifa  kwamba, haieleweki hivyo inachangia kwa kiwango kikubwa kufeli kwa watoto.
Naye Mwalimu Bakari Mwaliko wa Shule ya Msingi Mabaranga, Tarafa ya Mswaki, alishauri Serikali kuwachunguza watu waliosahihisha mitihani ya wanafunzi wa msingi na sekondari, akihisi huenda kuna hujuma za kisiasa.