MAPANGO YA AMBONI
Mapango ya Amboni yako katika eneo la Kiamoni, kata ya kiamoni, tarafa
ya chumbageni, wilaya ya tanga, mkoa wa tanga. Ni eneo zuri la
kupumzikia, kwa tafi za kihistoria, kijiografia, kijiolojia, n.k
Mapango haya yako umbali wa kilomita 8 toka tanga mjini kupitia
barabara kuu inayoelekea Mombasa. Unaweza kufika katika hifadhi ya
mapango kwa kupitia mojawapo ya njia zinazoelekea huko. Ya kwanza ni
barabara ya changarawe iliyo upande wa kushoto meta 200 baada ya kuvuka
daraja la hofu, ya pili iko kilometa 1.5 kutoka daraja la utofu katika
kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu. Njia zote zinapitia katikati ya
kijiji cha kiamoni.
Mapango haya yametokana na mabadiliko ya nguvu za asili zilizobadilisha maumbile ya miamba ya chokaa kipindi cha jurasiki (
Jurassic period)
kama miaka inayosadikiwa kuwa zaidi ya milioni 150 iliyopita. Kulingana
na tafiti zilizokwishafanywa, eneo hili la mapango lilikuwwa tena chini
ya maji miaka milioni 20 iliyopita na linakadiriwa kuwa na ukubwa wa
kilometa za mraba 234 lenye mazingira ya miamba ya chokaa. Ni eneo
ambalo linapitiwa na mito na limejaa uoto wa asili.
Miamba ya chokaaa kwa asili huundwa na madini ya kashiamu kabonate [
Calcium carbonate=CaCo3].
Miamba hii ni migumu kumomonyolewa na maji ya kawaida, lakini ni rahisi
kuyeyushwa na maji yenye kiasi kidogo cha tindikali ya kaboni (
Carbonic Acid).
Tindikali ya kaboni iliyobadilisha maumbile ya miamba hii kwa
kumomonyoa na kusababisha mapango yaweza kutokana na maji ya mvua
yanapochanganyika na dioksidi ya kaboni (
carbodioxide) hewani
kabla ya kufika ardhini au na dioksidi ya kaboni inayopatikana ardhini.
Maji yanapojipenyeza ardhini huendelea kupokea dioksidi ya kaboni kutoka
muozo wa viumbe hai kama mimea na wanyama na kutengeneza tindikali.
Tindikali ya kaboni inapopambana na madini ya kashiamu kaboneti (
calcium carbonate)
katika miamba ya chokaa husababisha kumomonyoka kwa miamba hii katika
maeneo mbalimbali na kusababisha mapango. Mabadiliko haya huitwa
kabonesheni (
carbonation). Angalia mchanganuo wa kemikali ufuatao.
Wataalam wanaelezea njia mbalimbali zilizosababisha mapango katika eneo hili.
Kulingana na utafiti uliofanywa na mturi (
1979), njia ya kwanza ni ile ya maji ya mvua yanapochanganyika na hewa ya “
Carbondioxide” katika anga na kutengeneza tindikali (
carbonic acid)
ambayo inauwezo wa kuyeyusha madini ya calcium carbonate yanaunda
sehemu kubwa ya miamba ya chokaa. Maji haya yenye tindikali husababisha
mabadiliko kidogo yanapotelemka kuelekea ardhini. Yakifikia meza ya maji
(
water table) huku yakiendelea kuongezeka huzidi kuchanganyika na
carbondioxide) iliyoko kwenye maji ardhini.
Kina cha maji kikiongezeka maji haya yenye tindikali huwa na uwezo
wa kuyeyusha maungio ya miamba katika sehemu laini zaidi za miamba na
kusababisha nyufa. Nyufa hizi huzidi kupanuliwa na maji yanayotembea na
kusababisha baadhi ya mawe kuporomoka na kufanya mapango. Kasi ya maji
inapozidi njia ndogondogo hupanuliwa na kuwa kubwa zaidi na upo
uwezekano mapango madogo madogo hupanuliwa na kuwa kubwa zaidi na upo
uwezekano mapango madogo madogo kuunganishwa na hatimaye kuwa na
mfululizo wa mapango kama yanavyoonekana katika eneo hili.
Kina cha maji kinapopungua eneo huachwa likiwa kavu, lakini
mabadiliko hayo huweza kuendelea kutokea chini zaidi na kusababisha njia
na mapango mengine katika kina kingine ambapo hutokea muunganiko wa
mapango kwa baadhi ya maeneo.
Njia nyingine ni pale ambapo inasemekana eneo hili lilikuwa chini ya
usawa wa bahari yaani pembeni ya ufuko wa bahari. Mawimbi ya bahari
yakamomonyoa miamba ya chokaa na kusababisha mapango. Baada ya bahari
kurudi nyuma kutokana na kupungua kwa kina chake katika eneo hili, eneo
la mapango likaachwa likiwa kavu.
Njia zote zilizoelezwa zimehusika katika kutokea kwa mapango haya,
Mapango ya kwanza yatakuwa yalitokana na mmomonyoko wa miamba ya chokaa
kutoka na maji ya ardhini yenye tindikali yaliyoyeyusha maungio ya
miamba ya chokaa na kusababisha mapango. Kina cha bahari kilipopanda,
maji ya bahari yalifikia eneo la mapango na mawimbi yake kusababisha
kupanuliwa kwa mapango au mabadiliko katika kuta za nje na ndani ya
mapango. Kina cha bahari kiliposhuka, eneo la mapango kilikuwa chini
sana, maji ya mvua yenye tindikali yamekuwa na uwezo wa kuendelea
kupanua na kubadilisha mfumo wa mapango.
Haijulikani mapango haya yaligunduliwa lini, bali taarifa zilizopo
zinaonesha kwamba watu wa makabila yaliyoishi jirani na eneo la mapango:
Wabondei, Wasambaa, Wadigo, na Wasegeju wamekuwa wakiya tumia kwa ajili
ya matambiko ya mizimu tangu karne ya
16. Eneo hili la mapango kwa wakati huo lilijulikana kama eneo la mzimu wa mabavu.
Watu wanaamini habari za nguvu za mizimu katika kutatua matatizo ya
uzazi, kuongeza kipato, magonjwa n.k. Kwa hivi sasa hutoka sehemu mbali
mbali za Afrika Mashariki na kuja kuomba au kutambikia mizimu katika
vijipango mbali mbali. Mbali na matumizi hayo, kampuni ya kigeni
iliyojulikana kama “Amboni Limited” ilimiliki mashamba ya mkonge katika
eneo la ta nga na kuweka eneo hili chini ya himaya yake mwaka
1892
ili kulitumia kama sehemu ya kupumzikia. Hii inatokana na mazingira
mazuri na yenye utulivu ya mapango ya Amboni. Baadaye kampuni hii
ilijulisha serikali kuhusu kuwepo kwa mapango haya. Serikali ilichukua
hatua kutangaza eneo la mapango kuwa eneo la hifadhi mwaka
1922.
Mwaka 1937 ilipitishwa sheria ya mambo ya kale (
Monuments Preservation Ordinace of 1937) iliyofuatiwa na ile ya
1953 (
Monuments Preservation Ordinace of 1953) ambayo ingesaidia kulinda mambo ya kale ikiwa ni pamoja na mapango ya amboni. Mwaka
1963 serikali ya Tanganyika ikayaweka mapango chini ya usimamizi wa idara ya mambo ya kale. Mwaka
1964 serikali ilisimamisha sheria ya kikoloni ya
1937 na
1953 na kupitisha sheria ya mambo ya kale ya mwaka huo (
The Antiquities Act of 1964) iliyofanyiwa marekebisho mwaka
1979 (
Amendments Acts of 1979)
kwa ajili ya kulinda mambo ya kale nchini. Kwa upande wa mapango ya
Amboni, mbali na mambo mengine sheria inakataza kuandika au kuchora
kwenye kuta za mapango.
VIVUTIO:
- Kuna maeneo maalum yaliyotengwa kwa
ajili ya kuomba au kutambikia mizimu ambapo utaona vitu vingi
vinavyohusiana na imani za kijadi.
- Kuna miamba yenye maumbo ya kuvutia yanayofanana na Sofa/Kochi,
Meli, Mamba, Tembo, Sanamu ya bikira maria n.k. Kuna vitu vinavyoonekana
kama michoro inayofanana na unyayo wa mguu wa binadamu, na mnyama
inayotokana na uchafu, hasa vumbi na udongo ambao hunywea pamoja na maji
ya mvua na hatimaye kuganda katika paa la pango. Alama nyingine ni zile
zilizosababishwa na popo wanaoishi mapangoni.
- Kuna miamba inayokua au kuongezeka (Speleothems/Dripstones)
kutokana na mabadiliko ya kikemikali katika miamba ya chokaa.
Mabadiliko haya hutokana na maji yenye tindikali kuyeyusha madini ya “Calicium Carbonate”, kuyahamisha na kuya rundika katika eneo jingine. Mtokeo ni kupata miamba inayokuwa kutoka juu kuelekea chini (stalactite) au inayoelekea juu (stalagmite). Kulingana na utafiti uliofanywa na Mapunda na Msemwa (2005:101).
Miamba ya aina hii huongezeka/kukua kwa kasi zaidi kipindi cha mvua
kuliko kipindi cha kiangazi. Katika miaka kumi iliyopita, ukuaji wa
miamba ya aina hii ni milimeta 0.5 kila baada ya miaka 100. Na kwamba iliwahi kuongezeka kwa kasi ya milimeta 7 katika kila miaka 100 kipindi cha kati ya miaka 38,000 na 34,000 (38 & 34 Ka)
Yapo masimulizi mengine yanayohusu mapango haya, mfano:
Kuna simulizi zinazoelezea njia za mapango zinazoelekea
Mombasa, Maweni, Mkoa wa Kilimanjaro n.k. Vile vile zipo simulizi za
Osale Otango (
Samuel Otango) na (
Paulo Hamis). Watu hawa waliwahi kutumia kituo namba tatu ndani ya pango kubwa kama sehemu yao ya kujificha kati ya mwaka
1952 na
1956
huku wakiendesha harakati za kupambana na walowezi waliokuwa wamewekeza
katika maeneo ya Tanga. Walipora mali na kutishia maisha ya walowezi
katika maeneo mbalimbali. Serikali ya kikoloni iliwatambua kama wahalifu
na kujaribu kuwakamata bila mafanikio kwa kipindi kirefu. Mwaka
1957
Paulo Hamis alipigwa risasi maeneo ya Lushoto na kufariki. Wananchi wa
kawaida wanawakumbuka kama mashujaa walioendesha harakati za ukombozi wa
watu wanyonge kutoka katika mikono ya walowezi na watawala wa kikoloni.
NUKUU:
Habari hizi zimeandikwa kutokana na masimulizi pia maelezo kutoka katika vitabu mbalimbali