Sunday, December 30, 2012

Dijitali Kuanzia Dar Pekee,Mwanza, Tanga, Mbeya baadaye

Wananchi wakiwa kwenye foleni ya kununua ving'amuzi vya Startimes eneo la Bamaga jijini Dar es Salaam jana katika siku za mwisho kabla Mamlaka ya Mawasiliano nchini (Tcra) kuhamisha matangazo ya televisheni kutoka mfumo wa Analojia kwenda digitali.Picha na Silvan Kiwale



WAKATI zimebakia saa 24 Tanzania kuungana na nchi nyingine duniani kuanza kurusha matangazo ya televisheni kwa mfumo wa Dijitali zikiachana na ule wa Analojia, imebainika kuwa mpango huo utaanzia Mkoa wa Dar es Salaam pekee.
Habari za ndani kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), zilizolifikia Mwananchi Jumapili, zinaeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam pekee, ndiyo litakuwa la kwanza kuingia kwenye mfumo huo kuanzia Januari mosi, 2013 na siyo mikoa mingine nchini.
TCRA, imeshatangaza kuwa itaufunga mfumo wa analojia ifikapo Desemba 31 mwaka huu yaani kesho.
Habari hizo zimeeleza kuwa mamlaka hiyo imeamua kuchukua hatua za tahadhari katika utekelezaji wa mpango huo muhimu, kwa kuanza na mji mmoja baada ya mwingine, ambapo  mwezi mmoja baada ya Dar es Salaam kuanza kutumia mfumo wa dijitali, utafuatia Mkoa wa Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alipoulizwa aliliambia gazeti hili jana kwamba mamlaka yake itatoa ufafanuzi kuhusu suala hilo leo katika mkutano wake na waandishi wa habari.
“Hatuwezi kukurupuka katika suala hili, tuko makini, lakini kesho (leo), tutakuwa na mkutano wa wanahabari kwa ajili ya kueleza mikakati mbalimbali na jinsi tulivyojipanga katika jambo hili,” alisema Profesa Nkoma.
Tayari TCRA imetaja miji mingine mbali ya Dar es Salaam ambayo imeshaunganishwa katika mfumo wa dijitali kuwa ni pamoja na Arusha, Mwanza, Tanga, Mbeya, Moshi na kwa sasa mji wa Morogoro unajengewa miundombinu husika.
Habari zaidi zilieleza kuwa kwa utaratibu uliopo sasa itachukua miezi kadhaa kabla ya kuzimwa kwa mfumo wa analojia katika miji minane ya awali, ambapo pia itachukua muda mrefu zaidi kuzimwa mfumo huo nchi nzima.
Shirika la Kimataifa la Mawasiliano (ITU), limezitaka nchi zote duniani kuhamia kwenye mfumo huo wa kurusha matangazo ya televisheni wa dijitali kutoka mfumo wa analojia ifikapo Julai 2015.
Ikiwa nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Tanzania imeanza kutekeleza azimio la nchi hizo ilizozitaka kufanya hivyo mwaka huu wa 2012, badala ya kusubiri hadi tarehe ya mwisho iliyowekwa na ITU.  
Wakati Tanzania ikiwa mstari wa mbele kuhamia kwenye mfumo huo wa dijitali, ingawa kwa mtindo wa awamu, nchi nyingine wanachama wa EAC hasa Kenya na Uganda bado hazijaingia katika mfumo huo.
TCRA imezikabidhi kampuni tatu kufanya kazi ya usambazaji wa mfumo huo wa dijitali, ambazo ni Basic Transmissions  inayoundwa na Kampuni za IPP Media na Sahara
Communications, Kampuni ya Ting ya Agape Associates na Star Media Tanzania Limited (Startimes) ambayo ina ubia na  Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Star Communications and Technology ya China.
TCRA imekuwa ikielezea kuwa Tanzania ipo tayari kujiunga na mfumo huo kwa kuwa asilimia kati ya 22 kati ya 24 ya nchi ambayo inatumia analojia, tayari imefikiwa na mtandao wa mfumo wa dijitali, ikijumuisha miji minane ambayo kwa kiasi kikubwa kampuni ya Startimes imeifikia.
Hata hivyo, utata bado unagubika urushaji huo wa chaneli za bure ambazo ni ITV, Star TV, TBC1, Channel Ten na Eat Africa TV ikielezwa kuwa wamiliki wa vituo hivyo hawataki zionyeshwe bure kwenye kila king’amuzi bali ving’amuzi vyao pekee.

MKUU wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Muhingo Rweyemamu, ametangaza kufunga ofisi yake kuanzia Januari 3, mwakani hadi Februari 3, atangaza kuhamia kwa wananchi mwezi mzima

 
Amesema lengo la hatua ni kusimamia kwa vitendo miradi inayohusu kilimo, elimu na ardhi, lengo ikiwa ni kuwaletea wananchi maendeleo.Muhingo katika mahojiano na simu na gazeti hili jana, alisema atatumia muda huo wa mwezi mmoja kusimamia kazi za maendeleo akianza na suala la kuhakikisha vyumba vya madarasa vinapatikana kwa ajili ya kuchukua wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza na wanaojiunga na kidato cha kwanza. “Nitatembea katika tarafa zote saba za wilaya yetu.Nimemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya anipatie kila idara zinazohusika ofisa wa kuwa naye katika kazi hii. Kwa hiyo, nitakuwa na watu wa elimu, ardhi, kilimo, ufugaji wa nyuki na masuala ya wafugaji na wakulima.“Tunaanza na hili la madarasa kwa sababu sitaki mwanafunzi hata mmoja abaki nyumbani kwa kukosa madarasa ya darasa la kwanza na wale waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza,” alisema Muhingo ambaye kitaaluma ni mwalimu na mwandishi wa habari. Alisema katika kilimo, pia wataanza na shule 10 zilizoteuliwa kwa ajili ya kuendesha kilimo cha kisasa na hapo watatumia vocha 300 walizopewa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kila shule itakuwa na ekari 10, hivyo kufanya ekari 100. Alisema vocha hizo ni za mbegu, mbolea ya kupandia na kukuzia.Alisema mbali ya kupanda mahindi, pia shule hizo zitapanda mazao ya jamii ya mikunde na nia itakuwa ni kuhakikisha shule zinajitosheleza kwa chakula kwa ajili ya wanafunzi wake. “Namshukuru Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo kwa kutuletea vocha 300. Zitatusaidia sana. Ninataka Handeni inakuwa mfano katika mapinduzi ya kilimo, tukiamua tunaweza,” alisema Muhingo na kubainisha kuwa katika suala la kilimo, baadaye atakuwa na ziara wilayani Bagamoyo mkoani Pwani kujifunza kilimo cha mananasi.

Mbowe Amtangaza Dr Slaa Mgombea Urais 2015

KUMEKUCHA CHADEMA,Mbowe Amtangaza Dr Slaa Mgombea Urais 2015

CHANZO: Mtandao wa Wanabidii

Katika Mkutano Mmoja huko Karatu mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe amemtangaza Dr:W.P.Slaa kama mgombea urais kwa tiketi ya CHADEMA mwaka 2015 .


JK Amtembelea Padri Ambrose Mkenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar anayeuguza majeraha katika taasisi ya mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam
https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEiO7OtpGNtAxYOD58-ac8hsxussCFFZNJrw5zqD7MMuAR0oGBfun9rOdytebDOknmzdTgUyhj3uez5oQpyzbl0uPBuNweIcIL52b9CcDssjLLsychVdQhaE2h79jJ6YQwk4ppdHmx5Xy8h2/s1600/pd11568631345.jpg

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimsikiliza Padri Ambros Mkenda wa Kanisa Katoliki la Mpendae mjini Zanzibar anayeuguza majeraha katika taasisi ya mifupa ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Moi) jijijini Dar es salaam jana Jumamosi Dsemba 29, 2012 kukupigwa risasi sehemu za mdomoni na watu wasiojulikana mapema wiki hii wakati akisubiri kufunguliwa geti la nyumbani kwake maeneo Kitomondo Mjini Zanzibar akiwa ndani ya gari aliyokuwa akiendesha akiwa pekee yake. Rais Kikwete amempa Padri Mkenda pole nyingi na kumuombea apate nafuu haraka.