Marko Gideon
PANGANI, TANGA, Julai 15, 2011 (IPS) - Pangani siyo wilaya mpya
nchini Tanzania. Wengi wanatambua wilaya ya Pangani kuwa moja ya
wilaya zilizoanzishwa miaka mingi na moja ya vitovu vya ukoloni
na biashara nchini Tanzania. Mji wa Pangani uliopo katika eneo
Mto Pangani unapomwaga maji yake katika Bahari ya Hindi, upo
umbali wa takribani Kilomita 42 kutoka Tanga mjini.
Unapoingia katika mji wa Pangani unapokelewa na vitu vingi
ambavyo kama ni mgeni lazima utashangaa. Miongoni mwa vitu hivyo
ni majengo ya zamani ambayo yana historia ya ukoloni. Moja ya
majengo hayo ni lile linalotumika kama ofisi ya Mkuu wa Wilaya
hiyo. Umbali wa takribani mita mia mbili kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika
mji huu mdogo unaokadiriwa kuwa na wakazi elfu hamsini, unakutana
na mandhari nzuri ya Mto Pangani unavyomwaga maji yake katika
Bahari ya Hindi. Kandokando mwa mto huo mkubwa kuna barabara
ambayo imepangiliwa vizuri pamoja na kwamba imejaa mashimo ambayo
yanaashiria lami iliyotengenezwa wakati wa zama za mkoloni. Pia kuna majengo na bustani ambapo vyote hivyo vimepangiliwa vizuri na kuleta mandhari ya kupendeza ya mji huo mkongwe nchini.
Mbali na Mto Pangani na kuona majengo ya zamani, mgeni pia
ataona mabango yamebandikwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo
yakiwa na nembo ya UZIKWASA. Neno hili linasimama badala ya
shirika lisilokuwa la kiserikali katika wilaya hiyo lijulikanalo
kama Uzima kwa Sanaa.
TCMP ni shirika linalofanya kazi kwa kushirikiana na Kituo cha
Rasilimali za Pwani na Bahari (Coastal Resource Centre) chini ya
Chuo Kikuu cha Rhode Island nchini Marekani, serikali ya Tanzania
chini ya Shirika la Usimamizi wa Mazingira Tanzania (NEMC) na
kufadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo
ya Kimataifa la Marekani (USAID).
Pengine siyo jambo la kushangaza kuona kuwa wengi nchini
Tanzania wanahusisha suala zima la sanaa na uchezaji ngoma na
pengine michezo ya kuigiza au uchoraji. Lakini UZIKWASA
inatafsiri tofauti ya dhana hiyo ya sanaa.
Ndani ya moja ya ofisi zake tatu zilizopo kandokando mwa Mto
Pangani, shirika hilo limetandaza machapisho mbalimbali kuhusu
VVU na UKIMWI, elimu ya uzazi na kujamiiana kwa vijana, matumizi
ya kondomu, elimu ya malaria kwa watoto na wajawazito, magonjwa
ya ngono na ushauri nasaha na kupima VVU – yote haya yakifanya
kazi ya kuonyesha jinsi gani sanaa inaweza kuleta uzima.
Kwa mfano, unaweza kushuhudia machapisho yenye vichwa vya
habari kama vile "Maswali waliyouliza vijana kuhusu UKIMWI na
kizazi kipya", "Maswali waliyouliza vijana kuhusu mimba",
Mahusiano kati ya mwanaume na mwanamke", "Maswali waliyouliza
vijana kuhusu mahusiano ya kimwili", Maswali waliyouliza vijana
kuhusu matumizi ya kondomu", Walinde watoto na wajawazito dhidi
ya malaria", "Yafahamu magonjwa ya ngono na athari zake", "Mbinu
maalum za kumpa kijana kupambana na maisha", "Kuzuia maambukizo
ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto", "Fahamu ushauri nasaha
na kuchunguzwa maambukizo ya VVU na chapisho juu ya elimu ya
"Kuingia utu uzima".
Haya yote yanatoa picha kuwa UZIKWASA siyo shirika la
kufundisha uchezaji wa ngoma, bali linatumia aina zote za sanaa
ili kulinda maisha ya mwanadamu hasa vijana wa kike na wa kiume.
Moja ya shughuli za UZIKWASA ni kukabiliana na maambukizo ya
VVU/UKIMWI katika vijiji vya wilaya ya Pangani. Kazi hii
hufanywa kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi wa vijiji chini
ya Kamati za UKIMWI za Vijiji (Village Multi-sectoral AIDS
Committees-VMAC). Na moja ya shughuli za shirika hapa ni kutoa
elimu ya jinsi ya kukabiliana na VVU/UKIMWI na pia kusambaza
kondomu kwa walengwa ambao miongoni mwao ni pamoja na kundi la
wavuvi ambalo linaonekana kuwa katika hatari ya kuambukizwa
VVU/UKIMWI kutokana na asili ya kazi zao.
Kazi zao zinawafanya kuwa mbali na nyumbani kwa muda mrefu
ambapo huishi kwenye makambi. Wavuvi wa kiume na kike wanapokuwa
makambini wanaweza kuanzisha tabia hatarishi,Tabia hatarishi pia zinaweza
kujitokeza wakati wavuvi wa kiume wanapokutana na wanawake na mabinti wanaokwenda kununua samaki kwa ajili ya uchuuzi."
Utafiti wa kubainisha maeneo yanayosambaza kondomu ulioendeshwa
na UZIKWASA uliweza kujua nani wanauza kondomu, idadi ya kondomu
zinazouzwa kwa siku, kwa nini wengine hawauzi kondomu na kama
wanapenda kuuza siku zijazo.
UZIKWASA imepata mafanikio katika eneo hili. Kulingana na
maofisa wake viongozi wa kidini wanaonekana kukubali kuwa
VVU/UKIMWI haina dini. Hii imewafanya wasiendelee kuhubiri tena
dhidi ya kondomu wala kutetea matumizi yake.
"Wameendelea kuhubiri maadili mema kama njia nyingine ya
kujikinga na VVU/UKIMWI bila kugusia masuala ya matumizi ya
kondomu," anasema Urassa. Pia usiri uliogubika suala zima la
kuongelea kondomu mbele ya umma umeanza kuondoka. Kwa kiasi sasa
watu wanaweza kusimama mbele ya umati na kuendelea kuchangia
katika mjadala unaohusu matumizi ya kondomu.
Sanaa inayoleta uhai haishii kwenye kupambana na magonjwa
pekee, lakini pia kwenye kusaidia shughuli za kuongeza kipato
ili wananchi waweze kuendesha maisha yao bila shida. Hapa
unakutana na mradi wa Vikundi vya Kuweka na Kukopa (SACCOs). Kwa
sasa UZIKWASA inalenga katika kuhakikisha kuwa makundi yenye
matatizo zaidi katika jamii kama vile walemavu, yatima, wajane na
watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI yanajengewa uwezo wa
kuanzisha SACCOs zao au kujiunga na SACCOs zilizopo.