Tuesday, April 2, 2013

Kikwete: Sibagui dini yoyote nchini

 http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1736606/highRes/484917/-/maxw/600/-/elgirl/-/jk.jpg
Rais Jakaya Mrisho Kikwete

Rais Kikwete alisema hayo juzi katika hotuba yake ya ambayo huisoma kila mwishoni mwa mwezi, kauli ambayo imekuja wakati kukiwa na malalamiko kwamba Serikali imekuwa ikifumbia macho matukio ya uhalifu wenye sura ya uhasama wa kidini.

“Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo,” aliongeza Rais Kikwete.

Alisema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakisema nchi inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo na kwamba amekuwa akipendelea kushiriki zaidi katika shughuli za Kikristo kuliko za Waislamu.
“Naambiwa kuwa niko mwepesi kushiriki maziko ya maaskofu kuliko ya masheikh wanapofariki.

“Kuna misikiti mitatu ya Jijini Dar es Salaam ambayo iliwahi kunisomea itikafu ili nife kwa sababu za kubagua dini yao.
“Katika itikafu hiyo waliwajumuisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova,” alieleza Kikwete.
“Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa maaskofu na watu mbalimbali Waislamu na Wakristo,” alisema.

Alifafanua pale ambapo hakushiriki mazishi ya sheikh au askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa na shughuli nyingine ambazo ni lazima zifanywe na yeye au taarifa ilikuwa ya muda mfupi.
“Waislamu desturi yetu ni kuzika mara mtu anapofariki, hicho ni kikwazo kwangu kushiriki mazishi ya masheikh hasa ikiwa ni nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali pamoja kwenda pengine siyo nyepesi,” alisema Kikwete.

Alisema pia Waislamu wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu, kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na Serikali haichukui hatua yoyote ya maana. Alisema imefika mahali viongozi na waumini wa dini hizo kubwa mbili kama hawatakubali kubadili mwelekeo wa sasa basi tunakoelekea ni kubaya
“Nchi yetu tutaivuruga na sifa yake ya miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kama ndugu itatoweka. Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro na hata vita ya wenyewe kwa wenyewe,” alisema Kikwete.

Alisema Serikali haifurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo ambao wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka katika matukio tofauti.
“Vyombo vya usalama vinatambua wajibu wao na kama havitimizi wajibu wao huo utakuwa ulegevu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya Serikali,” alisema Kikwete.

Aliongeza; “Mtakumbuka kuwa mara kadhaa nimewakumbusha wakuu wa mikoa, wilaya na vyombo vya usalama kuacha ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.”

Kikwete alisema kuuawa kwa viongozi wa dini na kuchomwa makanisa kusichukuliwe kama Serikali yake imeshindwa kulinda usalama wa raia wake.

“Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa nchini,” alisema Rais Kikwete.

Ajali ya Jengo la ghorofa lililoanguka

Kikwete alisema sheria zitafuata mkondo kwa waliosababisha kuanguka kwa jengo hilo baada ya uchunguzi unaofanywa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi.

Alisema watakaobainika kuhusika watatakiwa kufikishwa mahakamani ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni zao za kuendesha shughuli za ujenzi.

Alitaka mikoa yote nchini kujifunza katika ajali hiyo kwa kufuata kanuni za ujenzi ili kuondokana na maafa yanayoweza kujitokeza.