Serikali
kupitia Mamlaka ya EPZ imetenga eneo lenye ukubwa wa Hekta 1,363 katika
Mkoa wa Tanga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uthamini wa eneo husika
umekamilika.
Hayo
yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma wakati Waziri wa Uwekezaji, Mhe.
Mary Nagu akijibu swali la Mhe. Omari Rashidi Nundu kwa niaba ya Waziri
wa Viwanda na Biashara aliyetaka kujua ni matayarisho na utekelezaji upi
unafanywa na Serikali uweza kutekeleza azma hiyo katika kipindi cha
mwaka 2010-2015 na ni nini hatma ya Viwanda vya zamani ambavyo kwa muda
mrefu havifanyi kazi.
Mhe.
Nagu amesema kuwa mkakati wa kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa jiji la
viwanda upo katika hatua nzuri na kuongeza kuwa kwa hivi sasa viwanda
vipya vilivyojengwa na vinavyojengwa ni pamoja na kiwanda cha NILCANT
cha kutengeza chokaa, kiwanda cha Rhino Cement pamoja na kiwanda cha
Sungura Cement ambacho kinatarajiwa kujengwa.
“Jiji
la Tanga limeingia ubia na kampuni ya Korea (GoodPM) kwa ajili ya
kutekeleza mradi mkubwa wa kujenga viwanda 15 katika eneo la ekari 73
huko Pongwe unaotarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu chini ya utaratibu
wa Tanga Economic Corridor”. Alisema Waziri Nagu.
Akijibu
swali la nyongeza toka kwa Mhe. Nundu lililotaka kujua kama Serikali
iko tayari kufanya tathmini kufufua viwanda vya zamani, Waziri Nagu
amesema kuwa Serikali inakubaliana na hilo na iko tayari kuhakikisha
viwanda hivyo vinafufuliwa.
Aidha
Mhe. Nagu aliongeza kuwa Serikali ni moja hivyo itashirikiana na Wizara
ya Viwanda kupitia Waziri wa Viwanda kuhakikisha kuwa viwanda vya
zamani vinafufuliwa.