Saturday, March 9, 2013

vigogo wavuliwa madaraka TBS

Profesa Mhilu alisema hatua hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kufanya usaili kwa vigogo mbalimbali wa shirika hilo
http://www.mwananchi.co.tz/image/view/-/1714304/highRes/473595/-/maxw/600/-/no9v67z/-/tbss.jpg'

 Profesa Mhilu alisema hatua hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kufanya usaili kwa vigogo mbalimbali wa shirika hilo,Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Cuthbert Mhilu alisema jana kuwa waliovuliwa madaraka ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora, Dominic Mwakangale na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Vifungashio, Kezia Mbwambo.
 Baada ya hatua hiyo, bodi hiyo ilimteua Tumaini Mtitu kuwa Mkurugenzi mpya wa Udhibiti Ubora na Agnes Mneney kuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Vifungashio,Wengine walioteuliwa ni Emmanuel Ntelya atakayekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Shirika na Edna Ndumbaro kuwa Meneja Uandaaji Viwango vya Uhandisi.
Kadhalika, Matrida Kasanga ameteuliwa kuwa Meneja wa Hati na Tehama na Anitha Kaveva anakuwa Meneja Mipango na Utawala.
Alipoulizwa kama hatua hiyo inakwenda sanjari na sifa baada ya kufanyika kwa usaili Profesa Mhilu alisema: “Ninachowaambia ni hicho... hakuna tatizo tulilobaini kuhusu viongozi hawa, haya ni mabadiliko ya kawaida.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Mbwambo alijibu kwa kifupi: “Sifahamu, wasiliana na mwenyekiti wa bodi au  mkurugenzi mkuu ndiyo wenye nafasi ya kuzungumzia zaidi kuhusu hatua hiyo.”
Akizungumzia uteuzi huo, Profesa Mhilu alisema: “Hata hawa tuliowateua kushika nyadhifa hizo watambue kwamba tutawafuatilia kwa karibu tukiangalia utendaji wao, asiyefanya kazi kwa ufanisi atang’olewa.”
Alisema Bodi hiyo imetoa maagizo kwa Menejimenti ya TBS kuhakikisha kwamba inakomesha bidhaa feki, inafanya ukaguzi wa magari, pia kuhakikisha inaondoa urasimu wa upatikanaji wa leseni kwa wajasiriamali wadogo lakini kwa kuzingatia viwango vya bidhaa wanazotengeneza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko alisema kuwa amejipanga kushirikiana na menejimenti yake ikiwa ni pamoja na kukomesha makundi miongoni mwa wafanyakazi ili kuleta tija.
Tangu ilipozinduliwa, bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kusafisha safu za utawala za shirika hilo baada ya kuanza kwa kumvua madaraka Kaimu Mkurugenzi Mkuu Leandiri Kinabo na kumteua Masikitiko kabla ya kuitisha usaili upya wa wakurugenzi.