Saturday, December 29, 2012

Maalim Seif Ziarani Tanga,Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF anatarajiwa kuhutubia mikutano mitatu ya hadhara katika viwanja vya Tangamano, Kwadiboma Sokoni na Handeni.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bibi Chiku Galawa akimkaribisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika Mkoa huo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga.

 





 
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Tanga, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga.

 
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na wananchi mbali mbali waliojitokeza kumpokea wakati walipowasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na wananchi mbali mbali waliojitokeza kumpokea wakati walipowasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili. (Picha na Salmin Said, OMKR)


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema wananchi wanahitaji kuelimishwa zaidi juu ya uhifadhi wa mazingira ili waweze kuyalinda na kuepuka kuyachafua.
Amesema uchafuzi wa mazingira mara nyingi umekuwa ukisababishwa na wananchi wenyewe, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa wananchi kupatiwa elimu ya mazingira ili kuepusha uharibifu huo.
Maalim Seif ameeleza hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga bibi Chiku Galawa, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili.
Amesema iwapo wananchi wataelimishwa ipasavyo wataweza kujiepusha na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kukata miti kiholela bila ya kuzingatia athari za kimazingira.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga bibi Chiku Galawa amesema uharibifu wa mazingira ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa huo, jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa huo.
Amesema Serikali ya Mkoa huo inatafuta njia mbadala ya kutumia nishati nyengine ili kupunguza matumizi ya kuni ambayo yanachangia ukataji wa miti kiholela.
“Iwapo serikali itazuia matumizi ya makaa na kuni, serikali na wananchi watapata nafasi ya kufikiria nishati mbadala ya kutumia kwa ajili ya kupikia, lakini tukiendelea kutumia kuni mawazo yetu yatabakia hapo hapo tu na tutaendelea kutumia kuni kila siku”, alitanabahisha bibi Chiku.
Amesema ukataji wa miti kiholela katika Mkoa huo umekuwa ukichangia kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kuweko kwa upungufu wa mvua pamoja na kuongezeka kwa hali ya joto.
Hata hivyo bibi Chiku amesema Mkoa huo umepiga hatua kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya barabara.
Akiwa Mkoani Tanga, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF anatarajiwa kuhutubia mikutano mitatu ya hadhara katika viwanja vya Tangamano, Kwadiboma Sokoni na Handeni.
Hassan Hamad (OMKR)

UTAJIRI WA GESI ASILIA: TUWASIKILIZE WATANZANIA WA MTWARA NA LINDI TUSIPUUZE

Zitto Kabwe


Maandamano ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM. Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu (kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?.
Watu wa Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima. Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la hasha.
Sio dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini? 
Tumesahau kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya Tumbaku.
Lakini tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali huru ya Tanzania?
Tujiulize zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye Gesi asilia.

Magufuli Amteua Prof Ninatubu Lema Kuwa Mwenyekiti Wa Bodi (ERB)

Prof Ninatubu Lema kutoka Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET), kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB)

 
WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli amemteua  Prof Ninatubu Lema kutoka Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET), kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), uteuzi huo unaanzia Desemba 20 mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya Magufuli iliyosambazwa kweye vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, na kusainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Balozi Herbet Mrango, ilieleza kuwa uteuzi huo, utadumu kwa kipindi cha miaka mitatu hadi Desemba 20, 2015.
 
Kwa mujibu wa sheria Na. 15 ya mwaka 1997 ya mabadiliko madogo ya sehemu ya 3(3) ya kifungu 1(1) (a), na 1(2), kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 24 ya mwaka 2007, ndiyo iliyomfanya Waziri afanye uteuzi wa wajumbe wa Bodi hiyo akiwemo mwenyekiti huyo.
 
Katika uteuzi huo, Magufuli pia aliwataja wajumbe wanane wa bodi hiyo ya ERB, kuwa ni pamoja na Fintan Kilowoko kutoka wizara hiyo, ambapo kwa sasa ni mkurugenzi wa Barabara za Mikoa, Joseph Malongo, ambaye kwa sasa ni Msajili Msaidizi Huduma za Usajili na Gemma Modu kutoka Baraza la taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Nuberis Nyange kutoka Chama cha Wahandisi Washauri nchini (ACET).
 
Wengine ni Sarah Barahamoka, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Edwin Ngonyani kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Prof Bakari Mwinyiwiwa; Mhandisi Mwandamizi, Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET), kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Prof. John Kandoro; Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
 
Waziri alisema kuwa jukumu la msingi la Bodi hiyo ya Usajili wa Wahandisi ni kusajili wahandisi pamoja na Kampuni zinazotoa ushauri wa kihandisi, kuendeleza wahandisi kitaaluma, kuwajengea uwezo wa Wahandisi wa kitanzania.

Serikali Yaombwa Kuongeza Fedha Za Mkopo Wa Vijana

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo  wilayani Bukoba kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo  ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana.

 
Na: Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
 
Serikali imeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na baadhi ya  vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia  shamba lake la migimba na kahawa  ambalo  ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda  kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na  magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa  kikundi cha Msifuni  Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki tano  kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba  alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa  samaki  na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa   kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa samaki  ikiwa ni pamoja na kuibiwa  na kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema Joel.
Kwa upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza   kujishughulisha na kazi  za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana  ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu,  kufanya kazi si lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na mkiiuza mtapata fedha nahivyo  kujikwamua kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika ambao ni vijana watakuwa  tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha watayapata  na yatawasaidia katika maisha yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana  vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje  vijana kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la mfano la kahawa na migomba, kikundi cha burudani cha  Rugazi na  shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.

Taarifa Ya Wizara Juu Ya Mafuta Ya Diesel Feki


 JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
SERIKALI YAZUIA KUINGIZWA MAFUTA YA DIESELI YALIYO
CHINI YA KIWANGO NCHINI

Mwezi Novemba 2012, Kampuni ya Addax Energy SA ya Uswisi
ilishinda zabuni ya sita ya kuingiza mafuta kwa pamoja chini ya utaratibu
unaosimamiwa na Kampuni ya uagizaji mafuta kwa Pamoja (PICL).
Zabuni hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya mafuta ya Mwezi Desemba 2012 na
mwanzoni wa Januari 2013.

Utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja huzingatia pamoja na
mambo mengine viwango vya ubora wa mafuta kama vinavyoelekezwa na
Shirika la Viwango nchini (TBS). Aidha, TBS hukagua ubora wa mafuta
hayo kabla hayajaingia nchini.

Pamoja na aina nyingine za mafuta, Addax Energy SA ilipaswa kuleta
mafuta ya dieseli yenye ujazo wa MT 100,000 sawa na takriban lita
100,000,000 katika zabuni ya sita. Meli ya AL BURAG iliyobeba mafuta
hayo ilitakiwa kufika hapa nchini na kupakua mafuta kati ya tarehe 17
mpaka 20 Desemba 2012. Hata hivyo, meli hiyo ilifika tarehe 24 Desemba
2012 ikiwa imechelewa kwa siku nne kwa mujibu wa ratiba. Mafuta hayo
yalipimwa na TBS tarehe 26 Desemba 2012 na kugundulika kuwa yako
chini ya viwango vinavyotakiwa kwa Tanzania. Aidha, tarehe hiyo hiyo,
Kampuni binafsi ya Intertek Testing Services iliyoajiriwa na PICL pamoja na
Addax Energy SA ilipima mafuta hayo na kujiridhisha kuwa yalikuwa chini ya viwango vinavyotakiwa.

Kwa kuzingatia hali hiyo Serikali imechukua hatua zifuatazo:

1. Imeiagiza PICL pamoja
Addax Energy SA
IYARUDISHWE yalikotoka

2. Imeiagiza EWURA ichukuwe hatua stahiki za KISHERIA dhidi
ya Kampuni ya Addax Energy SA,

3. PICL ichukuwe hatua zinazotakiwa dhidi ya Kampuni ya Addax
Energy SA kulingana na MKATABA, na

4. Imeziagiza PICL pamnoja na EWURA kuhakikisha kuwa hali hii
haijirudii tena hapa nchini.

Aidha, Wizara ya Nishati na Madini inapenda kuwahakikishia wananchi
kuwa kutopokelewa kwa mafuta hayo yaliyo chini ya viwango
HAKUTAATHIRI upatikanaji wa mafuta ya dieseli nchini kwa kuwa kwa
sasa kuna mafuta ya kutosha.

Katibu Mkuu