Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli.
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Bungu wakiwa katika ofisi za walimu kuzungumzia mafanikio na changamoto mbalimbali kitaaluma katika shule hiyo.
Kibao cha Shule ya Sekondari ya Bungu.
Na Mwandishi wa Thehabari.com, Korogwe
SUALA la kuwepo na utata kwa baadhi ya
wanafunzi kukwamishwa na fomu namba 9 ya Takwimu za Shule za Msingi kwa
mwanafunzi (TSM9) kufanya mitihani yao katika shule anuai za sekondari
limezua mvutano kati ya wazazi wa wanafunzi na walimu huku kila upande
ukitupa lawama kwa mwenzake.
Baadhi ya wanafunzi na wazazi waliohojiwa wamedai uzembe upo kwa walimu
ambao hutumia majina ya wanafunzi wengine kuingiza wanafunzi kinyemela,
jambo ambalo huzua utata baadaye kwa mwanafunzi aliyeingia kwa njia hiyo
anapokaribia kufanya mitihani yake.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi wilayani Korogwe katika
shule kadhaa za sekondari na msingi umebaini kuwa wapo wanafunzi ambao
wamezuiwa kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne na ule wa kidato
cha pili wa mchujo kutokana na hali kama hiyo ya utata katika suala hilo
la TSM9.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bungu, Dismas Kimweli ambaye shule yake
ilikuwa miongoni mwa shule zilizolalamikiwa, akizungumza na mwandishi wa
habari hizi alipinga kuwepo na wanafunzi waliozuiliwa kufanya mitihani
yao kutokana na utata wa fomu namba 9.
Mwalimu huyo alisema idadi kubwa la wanafunzi ambao hukumbwa na matatizo
kama hayo ni wanafunzi ambao huingia shuleni kwa njia ya uhamisho huku
wazazi wao wakiomba mwanafunzi aendelee kusoma wakati utaratibu wa
kufuatilia uhamisho ukiendelea.
“Unakuta mzazi anamleta mtoto kujiunga na shule yako akitokea shule
nyingine na anaomba aendelee kusoma wakati akiendelea kufuatilia
uhamisho...lakini baadaye anakaa kimya sasa mtoto anakuwa anaendelea na
shule bila kuwa na uhamisho ambao hujumuisha TSM9, ikifika kipindi cha
mitihani hapo linakuwa tatizo na mzazi anajifanya kasahau,” alisema.
“Sasa kama mtu hajatimiza vitu kama hizi anarushaje lawama kwa walimu au
shule...lakini ikifikia hatua hii wapo ambao huwaeleza nao kuelewa na
wapo ambao huwa na mvutano kidogo,” aliongeza mwalimu huyo.
Akitoa ufafanuzi wa suala hilo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri
ya Wilaya ya Korogwe, Shaban Shemzighwa alikiri kuwepo kwa malalamiko ya
baadhi ya wanafunzi kutokuwa na TSM9 hasa wa kidato cha pili lakini
alidai waliruhusiwa kufanya mitihani yao na wao kuwaagiza wakuu wa shule
wanazotoka kuhakikisha wanawasilisha namba zao kwenye vituo
inakosahishiwa mitihani.
“Taarifa za malalamiko zilitufikia na baadhi ya Shule za Sekondari
ambazo wanafunzi walikuwa na matatizo hayo ni Bungu, Patema, Mfundia na
nyinginezo, hapa nipo nje ya kituo cha kazi hivyo ni vigumu kutaja idadi
na shule zote,” alisema Shemzighwa akizungumza na mwandishi wa habari
hizi kwa njia ya simu.
Aidha akifafanua zaidi alisema wanafunzi wengi waliokuwa na matatizo
kama hayo wa kidato cha pili ni wale waliohama kutoka shule moja kwenda
nyingine, ambao hawakuja na TSM9 zao. “…Hata hivyo waliruhusiwa kufanya
mitihani na maelekezo tuliwapa wakuu wa shule kuhakikisha wanapeleka
namba za wanafunzi hao katika kituo cha kusaishia mitihani ili waweze
kutambuliwa kihalali vinginevyo hawawezi kutambulika,” alisema ofisa
huyo.
Alisema inaonekana kuna baadhi ya walimu wakuu walipokea wanafunzi bila
TSM9, hata hivyo haikujulikana kama ni kwa njia ya kinyemela au matatizo
ya uhamisho kwa wanafunzi hao kutoka shule moja hadi nyingine. Hata
hivyo licha ya kiongozi huyu kuitaja Bungu kuwa miongoni mwa shule
zilizotolewa tarifa kuwa na tatizo la fomu namba 9, mkuu wa shule hiyo
alipinga shule yake kuwemo.
*Imeandaliwa na Thehabari.com kwa ushirikiano na HakiElimu