Tuesday, June 4, 2013

ENEO KUBWA KWA AJILI UFUFUAJI WA VIWANDA LATENGWA JIJINI TANGA

Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma.

Serikali kupitia Mamlaka ya EPZ imetenga eneo lenye ukubwa wa Hekta 1,363 katika Mkoa wa Tanga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na uthamini wa eneo husika umekamilika.

Hayo yamesemwa Bungeni Jijini Dodoma wakati Waziri wa Uwekezaji, Mhe. Mary Nagu akijibu swali la Mhe. Omari Rashidi Nundu kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara aliyetaka kujua ni matayarisho na utekelezaji upi unafanywa na Serikali  uweza kutekeleza azma hiyo katika kipindi cha mwaka 2010-2015 na ni nini hatma ya Viwanda vya zamani ambavyo kwa muda mrefu havifanyi kazi.
 Mhe. Nagu amesema kuwa mkakati wa kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa jiji la viwanda upo katika hatua nzuri na kuongeza kuwa kwa hivi sasa viwanda vipya vilivyojengwa na vinavyojengwa ni pamoja na kiwanda cha NILCANT cha kutengeza chokaa, kiwanda cha Rhino Cement pamoja na kiwanda cha Sungura Cement ambacho kinatarajiwa kujengwa.
“Jiji la Tanga limeingia ubia na kampuni ya Korea (GoodPM) kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kujenga viwanda 15 katika eneo la ekari 73 huko Pongwe unaotarajiwa kuanza mwezi Mei mwaka huu chini ya utaratibu wa Tanga Economic Corridor”. Alisema Waziri Nagu.
Akijibu swali la nyongeza toka kwa Mhe. Nundu lililotaka kujua kama Serikali iko tayari kufanya tathmini kufufua viwanda vya zamani, Waziri Nagu amesema kuwa Serikali inakubaliana na hilo na iko tayari kuhakikisha viwanda hivyo vinafufuliwa.
 Aidha Mhe. Nagu aliongeza kuwa Serikali ni moja hivyo itashirikiana na Wizara ya Viwanda kupitia Waziri wa Viwanda kuhakikisha kuwa viwanda vya zamani vinafufuliwa.