MCHEKESHAJI 'pacha' na marehemu Sharo Milionea, Musa Kitale 'Teja'
FAMILIA ya Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ aliyefariki dunia Novemba 26, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea Songa-Kibaoni, Muheza, Tanga imemteua msanii wa vichekesho Musa Kitale kuwa mwangalizi wa mali za marehemu.
Alisema
amepewa jukumu la kuhakikisha mikataba yote ambayo marehemu aliifanya
na makampuni mbalimbali inakwenda vizuri sanjari na kuangalia mali kama
vile gari na samani za ndani ya nyumba.
“Nimeambiwa
nisimamie mikataba, niangalie mali za mshikaji (Sharo) kwa kipindi
chote cha kusubiria arobaini ya marehemu ambayo itafanyika Januari 4,
2013 kijijini alikozikwa,” alisema Kitale.
Kitale
alisema baadhi ya mikataba anaifahamu kwa vile yeye ndiye aliyekuwa
shahidi, “lakini wa DTV aliosaini siku tano kabla ya kufariki dunia
(hakuutaja) inabidi aushughulikie Muddy Suma jamaa aliyemuazima gari
marehemu,” alisema.
Kuhusu kwenda kuzima taa katika nyumba aliyokuwa akiishi marehemu, Sinza Palestina Dar, Kitale alisema:
“Kwa
kipindi hiki ambacho tunasubiri arobaini ya marehemu ifike ni ngumu
mtu kwenda kufungua mlango ili azime taa, namuomba mama mwenye nyumba
avumilie kwani zoezi la kufungua mlango wa kwa Sharo ni hadi familia
yake iwepo hapa Dar na si mimi peke yangu.”
Akakumbuka
jambo hili: “Tulishtushwa na taarifa tulizozisoma kwenye Gazeti la
Risasi Jumamosi iliyopita kuwa, kuna rafiki mmoja wa marehemu alikwenda
pale nyumbani na kutaka kutapeli vitu vya marehemu, kama isingekuwa
msimamo wa mwenye nyumba jamaa angefanikisha utapeli wake ndiyo maana
haraka sana familia ikanipa mimi jukumu hili.”
No comments:
Post a Comment