Friday, December 7, 2012

KAMA HAUJAWAHI KUSIKIA AU KUFIKA TANGA

Kihistoria Mkoa wa Tanga ulitumiwa sana na wakoloni wa Kireno, Kiarabu, Kijerumani na Kiingereza ikiwa lango la biashara na uchumi kwa kuunganisha sehemu za ndani za Afrika Mashariki  na Kati na sehemu mbalimbali za Dunia
 
 hii ni ofisi ya mkuu wa mkoa wa tanga maeneo ya masiwani
 
kupitia bahari ya Hindi. Mwaka 1840 eneo  la  Manga  lilikuwa  njia  waliopitia wafanyabiashara  kutoka  Bara  Arabu  waliokuja kutafuta meno ya tembo  na  watumwa. Waarabu walikuwa wakiacha vyombo vya usafiri (majahazi) eneo la Sadani (Bagamoyo) na kuanza safari kupitia Manga, Kimbe hadi Kondoa Irangi. Misafara mingine ya  wafanyabiashara ilianzia Unguja kupitia Pangani, Kiwanda (Sindeni), Ngugwini, Mbego, Kwediboma, Mgera hadi Kondoa Irangi ambapo walileta nguo, shanga na vitu ili  kubadilishana  na  pembe  za ndovu, watumwa, chakula na mifungo. Kutokana na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali, wenyeji wa Tanga wamerithi tamaduni, lugha na ustaarabu  wa mataifa  mbalimbali ya Washirazi, Waarabu,  Wachina, Wahindi, Wareno, Wajerumani, Waingereza na Waswahili.
Mkoa wa Tanga ni mzizi na chimbuko la Tanganyika kabla ya kuungana na visiwa vya Unguja na Pemba mwaka 1964 na kuunda Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Tanganyika ilipata Uhuru mwaka 1961 huku Mkoa wa Tanga ukiwa ni msafirishaji mkubwa wa zao la Mkonge  duniani  na  mhimili  wa  kukua kwa uchumi  wa  nchi.  Jina  Tanga  lilitolewa  na wafanyabiashara  wa  Kishirazi  likiwa  na maana  nne  ambazo  ni  Tambarare,  Mabonde  ya Kijani, Barabara za Milimani na Kilimo cha  Milimani. Neno nyika ni la kibantu ambalo lilikuwa likitumiwa sana na wenyeji wakimaanisha mbuga au pori zaidi ya jina Tanga.
Harakati za kudai Uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza zilifanikiwa na Tanganyika kupata   Uhuru tarehe 9 Disemba, 1961 chini ya uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ndani ya chama cha TANU. Wakati huo (1961) Mkoa wa Tanga ulikuwa ni Jimbo lenye Wilaya tano (5) ambazo ni Wilaya ya Tanga, Handeni, Pangani, Usambara na Same.
 

No comments:

Post a Comment