Sunday, December 23, 2012

Katibu Bavicha Tanga ‘kukiona’

 
UONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani hapa, umeapa kumshughulikia ipasavyo Katibu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), mkoani Tanga, Deogratias Kisandu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Chadema mkoani humo, Saidi Mbwete alisema kitendo cha Katibu huyo kumtaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa ajiuzulu kwa kumiliki kadi ya CCM ni cha utovu wa nidhamu.
Mbwete alisema kauli na vitendo vya katibu huyo, vinaonyesha utovu wa nidhamu na kumdhalilisha Dk Slaa.
Alisema mtu anapohama chama kimoja na kujiunga na kingine, huwa amejitoa moja kwa moja kutoka kwenye chama chake cha awali.“Kurudisha kadi ya chama cha awali, ni hiari ya mwenye kumiliki kadi hiyo kwani ni yake kwa sababu ameinunua na kuilipia,” alisema Mbwete.
“Hata katiba za vyama vingi hazisemi kwamba mwanachama anapokihama chama chake, anatakiwa arudishe kadi,” alisisitiza
Mwenyekiti huyo alisema uongozi wa mkoa wa chama hicho, umekuwa ukifuatilia nyendo za kiongozi huyo wa Bavita na kugundua kuwa anatumiwa na CCM ili aivuruge Chadema.
“Tumegundua kuwa huyu si mwenzetu kwa sababu mawazo yake huwa kwake ni uamuzi ya kikao, ndiyo maana hata tangazo lake la kumkosoa Dk Slaa halikuwa na baraka za kikao,” alibainisha.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa wao kimkoa hawana mamlaka ya kumfukuza katika uongozi au uanachama isipokuwa watapeleka mapendekezo yao kwenye vikao vya ngazi ya juu kwa uamuzi wa mwisho.
Madai hayo ya kumshughulikia katibu huyo, yamekuja baada ya kutoa waraka unaomtaka Dk Slaa ajiuzulu kutokana na kumiliki kadi mbili za vyama vya siasa.

Na Raisa Said, Tanga

No comments:

Post a Comment