Friday, February 1, 2013

polisi Mtwara wakimbia makazi

Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)  katika ubishi Mtwara hivi karibuni

SHINIKIZO la wananchi mkoani Mtwara kutaka gesi isitoke mkoani humo, limesababisha polisi takriban 50 kuzikimbia familia zao baada ya kutishiwa maisha na wananchi.

Habari za kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Maria Nzuki zimeeleza kuwa polisi hao ambao wengi wao ni wale wanaoishi mitaa mbalimbali mjini humo, wamehamia kambini kutokana na kutishiwa maisha na wananchi kwamba watawadhuru wao na familia zao.

Habari hizo zilieleza kuwa, vurugu zilizotokea Januari 25 na 26, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu wanne huku jengo la Mahakama ya Mwanzo na nyumba zikiwamo za wabunge kuchomwa moto na nyingine kuharibiwa vibaya, ni moja ya sababu zilizowatisha polisi hao.
“Wamerudi kambini kwa sababu ya kutishiwa ila ni baadhi ya askari, siyo wote,” alisema kamanda huyo.

Juzi, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema hasira za wananchi hao ni kudhani kuwa gesi hiyo itapelekwa wilayani Bagamoyo nyumbani kwa Rais Jakaya Kikwete.
Alisema pia mpasuko ndani ya CCM mkoani humo na harakati za kisiasa ni sababu nyingine zilizochochea mgogoro huo.

Hata hivyo, Kamanda Njuki alisema hana idadi kamili ya askari waliokimbia makazi yao huku akifafanua kuwa mambo yatatulia mkoani humo ikiwa Serikali itatekeleza ahadi zake.
“Serikali inatakiwa kutekeleza ahadi zake ilizozitoa kwa wananchi ili kuweka hali shwari, lakini pamoja na hayo sisi tutaendelea na ulinzi kuhakikisha kuwa kila kitu kinakwenda sawa na hali inakuwa shwari,” alisema Njuki.

Alisema baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwatisha polisi hao na kutokana na hali hiyo imeonekana ni vyema waende kambini.

Askari wengi waliokimbia nyumba zao ni wale ambao makazi yao yanafahamika na wananchi ambao wakati wa vurugu hizo, walikuwa miongoni mwa askari waliokuwa waki zituliza. Inaelezwa kwamba wapo polisi zaidi ya 40 ambao hawaonekani mtaani na hata katika nyumba wanazoishi.

“Hivi sasa hawapo, si unaona mji ulivyokuwa mweupe, watu wana hasira na wanataka gesi isitoke, kwa hiyo hata wakimwona polisi wanaweza kumfanya lolote,” alisema mtoa habari ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini na kuongeza:

“Wananchi sasa wamekuwa kitu kimoja, wameweka siasa na tofauti zao nyingine kando kutaka gesi iwanufaishe, ila binafsi naomba jambo hili limalizike kwa amani.”

No comments:

Post a Comment