Thursday, October 25, 2012

Watumishi 15 Kilindi wapata msukosuku wa ubadhirifu

 https://encrypted-tbn0.gstatic.com/images?q=tbn:ANd9GcSbG9_EpcP0JDXBHXeQHky95ZATx8UL95Acdh_StyPdX1s2weMT
Hussein Semdoe, Kilindi
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ,mkoani Tanga, limewafuta kazi watumishi wawili  kati ya 15 wa halmashauri hiyo waliokuwa wakikambiliwa na utata wa ubadhirifu.

Watumishi wengine watatu kati ya hao wamevuliwa madaraka yao kwa madai ya kutiwa hatiani kwa makosa mbalimbali yaliyoisababishia hasara Serikali.
Watumishi hao waliochukuliwa hatua hizo ni miongoni mwa wafanyakazi 15, wa halmashauri hiyo, waliokuwa wakihusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma.
Madiwani hao walifikia uamuzi huo mwishoni mwa wiki katika kikao cha halmashauri hiyo maarufu kwa jina la ‘Waseuta Nougone’, kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wake Mussa Semdoe na Mkurugenzi Mtendaji Daudi Mayeji.

Awali, katika mkutano huo, Ofisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Pascal Lefi, aliwasilisha taarifa ya kamati ya uchunguzi wa watumishi waliokuwa na tuhuma mbalimbali kwa niaba ya Mkurugenzi, na kutaja majina ya watumishi 10 waliokuwa wamefunguliwa mashtaka ya nidhamu.
“Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ilikumbwa na tuhuma za ubadhilifu wa fedha za umma, hali iliyofanya uongozi  kuomba kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kuja kufanya ukaguzi maalumu, kwa hesabu za mwaka 2008, 2009 na 2010. Baada ya kukamilika ukaguzi huo jumla ya watumishi 15 walihusishwa na tuhuma hizo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza.
“Matokeo ya ukaguzi huo yamefanya watumishi watano wasimamishwe kazi na kupelekwa katika vyombo vya dola ama sheria, wengine wanne walisimamishwa kazi kupisha uchunguzi na watumishi wengine sita waliendelea na kazi huku tuhuma zikiendelea,” alisema Mkurugenzi huyo.
Mayeji aliwataja watumishi waliofutwa kazi kuwa ni Robert Kwayi, aliyekuwa ni mhasibu, ambaye ametiwa hatiani na kamati hiyo, kutokana na uzembe uliosababisha halmashauri hiyo kupata hasara ya Sh 80 milioni, na Edward Kapwapwa, ambaye ni Afisa Kilimo Msaidizi, aliyetimuliwa kazi kutokana na utoro kazini.
Aliwataja maofisa waliovuliwa madaraka, kuwa ni pamoja na, Fredrick Kiango, aliyekuwa Afisa Kilimo na mifugo wa Wilaya ya Kilindi, ambaye amekutwa na hatia ya Uzembe uliosababisha wilaya hiyo kupata hasara ya Sh 80 milioni, kwa kushindwa kushauri vizuri katika ununuzi wa Power Tiller zilizokuwa na upungufu.

No comments:

Post a Comment