Friday, December 28, 2012

Maamuzi Ya Baraza La Madaktari Juu Ya Madaktari Waliogoma

Kutokana na mgomo wa madaktari uliotokea kati ya tarehe 23 na 29 mwezi
juni 2012.Wizara iliwasilisha malalamiko kwenye Baraza la madaktari
Tanganyika ili lifanye uchunguzi kuhusu madaktari hao .Idadi ya
madaktari wote waliogoma walikuwa 394, kati yao madaktari 376 walikuwa
ni madaktari walio katika mafunzo kwa vitendo (Interns) kutoka
hospitali za Muhimbili, K.C.M.C. Bugando, Mbeya Rufaa, St.Francis -
Ifakara, Dodoma, Temeke, Mwananyamala, Amana, Haydom na Sekou Toure.
Aidha, Madaktari waajiriwa(Registrar) 18 walishiriki katika mgomo huo
kutoka hospitali ya Rufaa ya Mbeya.


 Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila
daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.  Adhabu hizo
zilikuwa katika makundi yafuatayo; onyo, onyo kali na kusimamishwa
udaktari kwa muda wa kati ya mwezi mmoja na miezi sita.Vile vile kuna
Madaktari ambao hawakuwa na hatia ya kushiriki katika mgomo na hivyo
walifutiwa mashtaka.

MCHANGANUO WA ADHABU


•       Waliofutiwa mashitaka madaktari 49

•       Waliopewa onyo  madaktari 223
•       Waliopewa onyo kali madaktari 66
•       Kusimamishwa kwa muda madaktari 30
•       Mashitaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa
kisheria madaktari 4
•       Mashitaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa
na Baraza madaktari 22

Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za

Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na
hatia mbele ya Baraza la Madaktari.   Wizara pia imeridhia kuwapa
Madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya
kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla
ya kuondolewa.  Hata hivyo fursa hii haitawahusu Madaktari wote
waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo
watakapomaliza kutumikia adhabu zao.

HITIMISHO

Kwa taarifa hii madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa
onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la
Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili  na kuruhusiwa kuendelea
na mafunzo kwa vitendo. Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar)
wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya ili kupewa
barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.  Barua hizi zitatolewa
kuanzia tarehe 2 Januari, 2013.Madaktari wote walio katika mafunzo kwa
vitendo wanatakiwa kuanza kazi katika vituo vyao vya awali  ifikapo
tarehe 14 Januari, 2013.Hakuna muda utakaoongezwa kwa kipindi
kilichobakia cha mafunzo kwa vitendo. Kwa wale wote waliopewa adhabu
wataanza kutumikia adhabu hizo kuanzia tarehe ya adhabu hiyo
ilivyotolewa.

Nsachris Mwamwaja

Msemaji
WIZARA YA AFYA NA USTAWI  WA JAMII
27/12/2012

No comments:

Post a Comment