Friday, December 28, 2012

Nguvu Ya Rangi Katika Biashara Zetu

Na: Albert Sanga, Iringa.
Leo nitawapitisha wajasiriamali katika somo muhimu kuhusu rangi. Je, unafahamu chimbuko la neno yeboyebo hapa nchini? Twende pamoja. Kampuni moja ya nchini Tanzania miaka michache iliyopita imewahi kutambulisha bidhaa zake za juisi zilizokuwa zikifahamika kama “Yebo” Juhudi kubwa iliwekwa katika matangazo kutoa taarifa kwa watumiaji kuhusu uwepo wa bidhaa hizo.

 Juisi ile ilikuwa ni ya rangi ya njano na katika matangazo ya kwenye televisheni walikuwa wakitumika watu waliokuwa wamevaa kandambili za plastiki zenye rangi ya njano. Kwa sababu kandambili hizo ndio kwanza zilikuwa zinaingia sokoni zikabatizwa jina la yebo yebo.

Haikuishia hapo, neno ‘yebo yebo’ likawa linapewa kwa kila kitu chochote kilichoonekana kutumia ama kuwa na rangi ya njano. Timu ya mpira ya Yanga ilikuwa mmoja wa waathirika wa hali hiyo kwani ilibatizwa jina la Yebo yebo! 

Yebo yebo likajipatia urasmi wa ‘kiaina’ kutumika kwa ajili ya kumaanisha kitu kinachopatikana kwa wingi, kisicho na thamani kubwa na kinachodharaulika. Sina uhakika kampuni husika ilichukua hatua gani baada ya hapo kujisalimisha na hatari ya bidhaa zao kuchukuliwa “poa” kutokana na matangazo waliyoyabuni.


Ukifuatilia maarifa katika sayansi ya biashara utabaini kuwa tatizo la kuzuka kwa neno ‘yebo yebo’ halikuwa katika kandambili za plastiki wala halikuwa katika ubora wa bidhaa (kwa maana ya juisi yenyewe ukitoa ufungashaji) bali tatizo lilianzia katika rangi ya njano. Rangi ya njano ilipelekea kuzaliwa kwa dhana ya uyebo yebo kutokana na namna inavyotafsiriwa katika ubongo wa mtu.

Unapoona bidhaa yeyote ikiwa imefungashiwa kwa rangi za aina Fulani basi ujue jambo hilo halifanyiki kwa bahati mbaya bali linabeba maana kwa mtumiaji hata kama mtumiaji hajijui kwa nini anatumia bidhaa za rangi fulani na asitumie za rangi nyingine. 

Ukiangalia soda ya Seven Up kutoka kampuni ya Pepsi pamoja na soda ya Sprite kutoka kampuni ya CocaCola utaona kuwa soda hizi zina rangi nyeupe lakini zinafungashwa katika chupa za kijani, kwa nini?

Katika nchi nyingi masikini ikiwemo Tanzania, makampuni na wajasiriamali wengi wamekuwa hawatilii mkazo suala la rangi katika biashara zao. Hii inajumuisha katika bidhaa, mazingira ya huduma pamoja na rangi zitumikazo katika majengo ya kufanyia hizo biashara. Kupuuza suala la umuhimu wa rangi katika biashara kumepelekea wafanyabiashara na makampuni mengi kushindwa kukubalika miongoni mwa watumiaji.

Si kila rangi inafaa kupakwa katika kuta za duka, si kila rangi inafaa kutumika katika kuandika maandishi kwenye vifungashio vya bidhaa. Umakini wa kuzingatia athari za rangi miongoni mwa watumiaji kunatajwa kuwa ni moja ya sababu zinazosababisha bidhaa kutoka nje ya Tanzania kupendwa ukilinganishwa na za hapa nyumbani.

Kimsingi rangi zimethibitishwa kuwa na uwezo wa kushawishi saikolojia pamoja na tabia za watu.  Mtaalamu mmoja wa saikolojia, Ward aliwahi kuulizwa njia za kuwezesha wafanyakazi kupunguza misongo wakiwa kazini.  Alijibu, “Haihitaji semina wala mafunzo, jambo la msingi ni kupaka rangi sahihi katika kuta za vyumba wanamofanyia kazi, ambayo itaweka hamasiko ama mfifio kwa mabadiliko yanayohitajika”

Kwa mujibu wa mtafiti mwingine wa mambo ya biashara katika masoko, Wexner, anabainisha kuwa rangi nyekundu kwa mfano inatajwa kuwa inaambatana na hisia za kuhamasika, machungwa inaambatana na kukatishwa tamaa na kudharauliwa.  Zambarau inaonesha hali ya kuthaminiwa, njano inawakilisha hali ya furaha, mzaha na kicheko na nyeusi inaonesha nguvu, umiliki na uimara.


Makampuni na biashara mbalimbali duniani kila siku zinakazana kutafuta njia za kuwezesha mwonekano na nguvu za nembo zao. Njia thabiti zinapovumbuliwa mikakati ya kimasoko huwekwa ambayo inahakikisha kuwa nembo hizo zinakuwa katika akili na fikra za wateja. 

Tofauti za kiutamaduni, kiuchumi, kijamii na nyinginezo zinaleta changamoto ya ugumu kwa biashara na makampuni kufahamu kwa usahihi aina moja tu ya nembo ambayo itawaridhisha na kuwapendezesha wateja wote. Hivyo biashara nyingi hasa za kimataifa zinajikuta kuwa zinalazimika kuwa na nembo moja katika muundo tofauti tofauti ili kufanikisha ufikaji wa bidhaa kama ilivyokusudiwa.


Mbinu mojawapo ya kimasoko inayotumika na waendeshaji wa masoko hasa kimataifa bila kujali eneo ama watu gani wanaoenda kutumia bidhaa hizo ni rangi. Rangi ni moja ya vifaa ambavyo mameneja masoko hutumia katika kutengeneza, kuimarisha na kurekebisha mwonekano wa nembo katika ufahamu wa mteja. Umuhimu wa rangi kuwasilisha maana Fulani kwa walengwa kunathibitishwa hata katika taratibu na sheria mbalimbali duniani.

Kwa mfano kule nchini Marekani kuna sheria inayofahamika kama Lanham Act ambayo inalinda rangi za bidhaa kama nembo halali za kibiashara . Rangi zinafahamika kuwa zinabeba chembechembe za kihisia na kisaikolojia. 

Maana mbalimbali zinazoambatana na rangi mbalimbali zinaumaana mkubwa sana kwa watu wanaohusika na masoko katika bidhaa ama huduma za makampuni mbalimbali, kwa sababu mbinu za kutangaza bidhaa ndizo huamua ukubalikaji wa bidhaa yenyewe.

Kwa mfano ua la waridi (rose) litabaki kuwa hivyo katika mataifa na tamaduni mbalimbali, lakini rangi za maua hayo zinakuwa na maana tofauti tofauti kutoka utamaduni, taifa moja kwenda jingine. Wajapan wanapendelea maua hayo yenye rangi nyeupe wakati watumiaji kutoka Hong Kong wanapendelea kutumia maua hayo ya rangi nyekundu

Mtu anapotaka kununua gari, rangi inatajwa na wataalamu wa masuala ya biashara kuwa inashika nafasi ya tatu katika orodha ya vigezo vya bei  na ubora . Rangi pia ina umuhimu mkubwa sana katika ujenzi wa nembo ikiwemo logo, ufungaji na uonyeshaji . 

Mtaalamu na mtafiti wa mambo ya masoko, Wagner kupitia taasisi yake ya utafiti wa mahusiano ya rangi na biashara, ijuliakanayo kama Wagner Color Research Institute, alijaribu kuthibitisha dhana yake  maarufu, ‘Colors are associated with certain images’ (rangi inaambatana na taswira fulani). Wagner alitumia kampuni inayoendesha migawaha iitwayo Wienerschnitzel yenye matawi zaidi ya 350 katika nchi ya Marekani. 

Wagner aliishauri kampuni hii kuongeza rangi ya njano kidogo katika rangi zinazopamba majengo ya migahawa yao ili kuwasilisha ujumbe kuwa kampuni hiyo kupitia matawi yake inauza vyakula vya bei rahisi. Baada ya kubadilisha rangi, kampuni hiyo iliripoti ongezeko la mauzo kwa asilimia saba.

Kiujumla rangi zinaambatana na taswira fulani  kila inapoonekana na kufikiriwa katika fikra za mteja. Kwa mfano rangi ya bluu mahali pengi huambatana na maana na taswira ya utajiri, uaminifu na usalama. Ndio maana ukifuatilia kwa umakini utagundua kuwa benki nyingi zinapenda kutumia ama kujumuisha rangi ya bluu katika nembo na machapisho yao. 

Hii inaingiza taswira miongoni mwa wateja wa mabenki hayo kuwa, benki ipo imara (utajiri mkubwa), ina umaninifu, (hivyo akaunti zake haziwezi kufanyiwa hujuma), na usalama, (kimbilio sahihi la kutunzia hazina zake). Wakati rangi ya njano inabeba mwonekano wa kitu cha bei rahisi

Wasimamizi wa masuala ya masoko katika makampuni na biashara wanapaswa kufahamu maana tofauti tofauti zinazoambatana na rangi ambapo maana hizo zitawezesha kugawanya na kupoka fursa mbalimbali za kimasoko kwenye jamii na tamaduni mbalimbali. Muunganiko wa rangi katika kufungasha bidhaa nao una umuhimu mkubwa sana ili kuwateka wateja.

Upo mfano mwingine wa kampuni ya kutengeneza vifaa vya kompyuta ya Apple kupitia bidhaa zake za iMac inafungasha kutumia mwunganiko wa rangi tano ambazo zina maana tofauti tofauti katika mataifa mbalimbali.  Rangi hizo ni kijani, dhahabu, nyeupe, bluu na njano. Bidhaa za iMac zinapoingia Taiwan zinatafsiriwa kuwa ni amani, rafiki (kijani), zisizo na madhara (bluu na nyeupe), endelevu (dhahabu), zinazosisimua, zinazofanya kazi kwa haraka na kwa ufanisi (njano). 

Muunganiko huo wa rangi unapoingia China tafsiri inakuwa ni nyingine kabisa lakini bado tafsiri inaisaidia na kuiwezesha kampuni kuuza bidhaa zake vizuri. Kule china bidhaa za iMac huleta maana ya; amani (kijani), nzuri na zinazoleta urembo (njano) wakati nyeupe huwakilisha vitu vilivyo katika mpangilio na vinavyofafanulika.

Kuna changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wa Tanzania hasa katika wakati huu ambao tupo katika jumuiya ya Afrika Mashariki. Namna bidhaa zetu zinavyotengenezwa na kufungashwa zinaamua sana jinsi zinavyoweza kushindana katika masoko ya kimataifa. 

Hata wafanyabiashara wadogo wadogo katika maduka na vibanda vyao ni vema sana wakawa na ufahamu wa namna ya kupaka rangi zitakazowavutia wateja na kuongeza uhakika wa kushinda changamoto za kiushindani!



No comments:

Post a Comment