JUMUIYA ya wanataaluma wa Kiislamu nchini (Tampro), imesema kwa kushirikiana na taasisi nyingine, inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha inawasaidia vijana wanaosoma katika shule za sekondari za Kata ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kama sehemu ya jitihada zao kwa jamii ya Watanzania.
Akizungumza kuhusu maazimio ya
mkutano mkuu wa jumuiya hiyo uliomalizika juzi katika hotel ya Lamada
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji Jumuiya hiyo Sadiki Gogo,
alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuridhika na utafiti ilioufanya na
kubaini kuna haja ya wao kama wanataaluma kutafuta njia ya kuwasaidia
vijana hao kimasomo.
”Tampro kupitia kliniki
yake ya Elimu, iliomba na kupata kibali Wizarani cha kufanya utafiti
katika shule kadhaa za sekondari za kata hapa nchini na kugundua kuwa
zina uwezo wa kufanya vizuri iwapo zitasaidiwa katika baadhi ya nyanja” alisema Gogo
Akifafanua baadhi ya nyanja
hizo, Mkurugenzi huyo, alisema pamoja na kuwapa mafunzo maalum walimu
wa shule hizo na baadae kupeleka walimu wa kujitolea katika baadhi ya
shule zitakazoonekana zina upungufu mkubwa.
Sambamba na mkakati huo ambao
amedai unalenga kuisaidia serikali, Gogo alisema Tampro kupitia mkutano
huo imeazimia kuanzisha vituo vya Elimu maalum pamoja na huduma
nyinginezo kwa watu wenye mahitaji maalum kama vile ya ulemavu.
Aidha Mkutano mkuu huo umeazimia
kushirikiana na wadau wengine nchini kuwekeza katika sekta ya Afya kwa
madai kuwa bila ya kuwa na watu wenye afya zilizoimarika ,ni ngumu Taifa
kufikia maendeleo ya kisiasa na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment