Saturday, December 29, 2012

Serikali Yaombwa Kuongeza Fedha Za Mkopo Wa Vijana

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  (kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo  wilayani Bukoba kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo  ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuvikopesha vikundi mbalimbali vya maendeleo vya vijana.

 
Na: Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
 
Serikali imeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya mkopo huo.
Ombi hilo limetolewa jana na baadhi ya  vijana waliopata mkopo huo kupitia SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa nyakati tofauti na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara  alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za ujasiriamali.
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia  shamba lake la migimba na kahawa  ambalo  ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda  kujifunza na kuchukua miche ya migomba.
Alisema kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba, bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika hasa soko la ndizi na  magonjwa ya migomba.
Naye katibu wa  kikundi cha Msifuni  Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa shilingi milioni moja na laki tano  kutoka Halmashauri ya wilaya ya Bukoba  alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima wa  samaki  na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu na wanampango wa kuhakikisha kuwa   kila mwanakikundi anakuwa na bwawa lake.
“Changamoto zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma kwa mradi wetu wa samaki  ikiwa ni pamoja na kuibiwa  na kuharibiwa kwa mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za maendeleo”, allisema Joel.
Kwa upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza   kujishughulisha na kazi  za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na nyuki.
Dk. Mukangara alisema, “Vijana  ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia ya uvivu,  kufanya kazi si lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe mwenyewe kama hapa Ibwera kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina miti mnaweza kuwa na mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao watawapatia asali na mkiiuza mtapata fedha nahivyo  kujikwamua kiuchumi”.
Kwa upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika ambao ni vijana watakuwa  tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo mengine kama ya uongozi, stadi za maisha watayapata  na yatawasaidia katika maisha yao.
Waziri Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na vikundi vya vijana  vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje  vijana kujikwamua kiuchumi. Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la mfano la kahawa na migomba, kikundi cha burudani cha  Rugazi na  shamba la samaki la kikundi cha Msifuni.

No comments:

Post a Comment