Saturday, December 29, 2012

Maalim Seif Ziarani Tanga,Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF anatarajiwa kuhutubia mikutano mitatu ya hadhara katika viwanja vya Tangamano, Kwadiboma Sokoni na Handeni.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Bibi Chiku Galawa akimkaribisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika Mkoa huo mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga.

 





 
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na vikosi vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Tanga, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga.

 
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na wananchi mbali mbali waliojitokeza kumpokea wakati walipowasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili. (Picha na Salmin Said, OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akisalimia na wananchi mbali mbali waliojitokeza kumpokea wakati walipowasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili. (Picha na Salmin Said, OMKR)


Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema wananchi wanahitaji kuelimishwa zaidi juu ya uhifadhi wa mazingira ili waweze kuyalinda na kuepuka kuyachafua.
Amesema uchafuzi wa mazingira mara nyingi umekuwa ukisababishwa na wananchi wenyewe, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita kwa wananchi kupatiwa elimu ya mazingira ili kuepusha uharibifu huo.
Maalim Seif ameeleza hayo wakati akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga bibi Chiku Galawa, mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Tanga kwa ziara ya siku mbili.
Amesema iwapo wananchi wataelimishwa ipasavyo wataweza kujiepusha na uharibifu wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kukata miti kiholela bila ya kuzingatia athari za kimazingira.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga bibi Chiku Galawa amesema uharibifu wa mazingira ni moja kati ya changamoto kubwa zinazoukabili Mkoa huo, jambo ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa huo.
Amesema Serikali ya Mkoa huo inatafuta njia mbadala ya kutumia nishati nyengine ili kupunguza matumizi ya kuni ambayo yanachangia ukataji wa miti kiholela.
“Iwapo serikali itazuia matumizi ya makaa na kuni, serikali na wananchi watapata nafasi ya kufikiria nishati mbadala ya kutumia kwa ajili ya kupikia, lakini tukiendelea kutumia kuni mawazo yetu yatabakia hapo hapo tu na tutaendelea kutumia kuni kila siku”, alitanabahisha bibi Chiku.
Amesema ukataji wa miti kiholela katika Mkoa huo umekuwa ukichangia kuwepo kwa athari za mabadiliko ya tabianchi yanayopelekea kuweko kwa upungufu wa mvua pamoja na kuongezeka kwa hali ya joto.
Hata hivyo bibi Chiku amesema Mkoa huo umepiga hatua kimaendeleo, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa miundombinu ya barabara.
Akiwa Mkoani Tanga, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF anatarajiwa kuhutubia mikutano mitatu ya hadhara katika viwanja vya Tangamano, Kwadiboma Sokoni na Handeni.
Hassan Hamad (OMKR)

No comments:

Post a Comment