Zitto Kabwe
Maandamano
ya amani yaliyofanyika mjini Mtwara siku ya alhamis wiki hii yameibua
hoja mbali mbali kutoka kwa viongozi, wananchi, vyombo vya habari na
mjadala wa siku nzima kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook, twitter
na JamiiForums. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameita waandamanaji wapuuzi na
Waziri wa Nishati na Madini amewaita watu hatari na wahaini. CHADEMA
tumetoa kauli kupitia kwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini kwamba
udhaifu wa utendaji serikalini ndio chanzo cha maandamano haya.
Lakini
kuna tatizo kubwa zaidi ambalo linaonekana siyo katika sekta hii tu bali
pia katika sekta nyingine ambapo tunaona matokeo yake katika maisha ya
watu wetu na naweza kusema ni dalili za kushindikana kwa sera za CCM.
Sera hizi ndizo ambazo zimelifikisha taifa hili hadi hapa. Kama hadi
wananchi wa Mtwara ambako kwa muda mrefu imekuwa ni ngombe ya CCM
wanaanza kuhoji matokeo ya sera za chama tawala basi ni dalili kuwa
Watanzania wamefungua macho yao na wanaona.
Wanaona
katika nishati, wanaona katika utawala bora, wanaona katia elimu
(kuanzia ya msingi hadi ya juu kabisa!), wanaona katika afya, wanaona
katika utendaji wa jeshi la polisi wanaona katika madini. Sera za CCM
zimeshindwa. Zimeshindwa kuinua maisha yao na zinaonekana kuendelea
kushindwa.
Mtwara na Lindi wanataka nini?.
Watu wa
Mtwara wanataka gesi isiondoke Mtwara na badala yake viwanda na mitambo
ijengwe Mtwara kisha kama ni umeme au mbolea isafirishwe kupelekwa
sehemu nyingine ya nchi. Watu wa Mtwara hawasemi kwamba Gesi yote na
mazao yake vibaki Mtwara na Lindi. Wanasema umeme uzalishwe Mtwara
usambazwe nchi nzima. Mbolea izalishwe Mtwara na kusambazwa nchi nzima.
Wanataka Bandari ya Mtwara iboreshwe na kuhudumia mikoa ya Kusini. Watu
wa Mtwara hawasemi kwamba mapato yote ya Gesi yatumike Mtwara tu la
hasha.
Sio
dhambi hata kidogo kwa watu wa Mtwara kudai masuala haya. Watu wa Mtwara
wamefanya maandamano kwa amani kabisa bila kuharibu mali na kutoa maoni
yao. Kwanini tuwasute na kuwasusubika kwa madai yao haya? Kwa nini
tusiwasikilize? Kosa lao nini kudai viwanda ili wapate ajira? Tumesahau
kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ni mikoa masikini kabisa nchini?
Tumesahau
kuwa mikoa ya Lindi na Mtwara ilitumika kwa ukombozi wa kusini mwa
Afrika kiasi cha kuwa katika hatari kabisa? Tumesahau ‘sacrifice’ ya
watu wa Mtwara na Lindi dhidi ya usalama wa nchi yetu? Tumesahau kuwa
Korosho imekuwa zao kubwa la biashara na linaloingiza mapato mengi sana
ya Fedha za kigeni? Waziri Muhongo anasema Mtwara warudishe Fedha za
Mkonge na Kahawa. Mbona hataji fedha za Korosho? Mwaka 2011 Korosho
ilikuwa zao la pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni baada ya
Tumbaku.
Lakini
tujiulize, watu wa Mtwara na Lindi walifadi fedha za Mkonge? Walifaidi
fedha za Kahawa? Wamefaidi fedha zao za Korosho? Tumesahau hata Reli
iliyoachwa na Mkoloni ya Nachingwea – Mtwara iling’olewa na Serikali
huru ya Tanzania?
Tujiulize
zaidi, hivi watu wa Nzega wamefaidika vipi na Mgodi wa Resolute pale
Lusu? Mgodi umefungwa ukiwa umezalisha na kuuaza dhahabu ya thamani ya
dola za marekani 3.3 bilioni. Hivi katika uhai wa mgodi huu Serikali Kuu
imekusanya kodi kiasi gani? Halmashauri ya Wilaya ya Nzega imepata
ushuru kiasi gani? Watu wa Mtwara wanayaona haya yaliyotokea Nzega na
yanayotokea Tarime, Biharamulo, Kahama na Geita. Watu wa Mtwara wana
Haki kuandamana kuzuia haya yaliyotokea wenzao yasiwatokee wao kwenye
Gesi asilia.
No comments:
Post a Comment