Wednesday, January 2, 2013

Dk Kigoda ambaye ni Waziri wa Viwanda na Biashara pia ni Mbunge wa Handeni akihutubia wananchi katika vijiji mbalimbali vya Kata za Kwamsisi, Kwasunga na Kwaluguru, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Dk Kigoda alisema kuwa, wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya kati ya 45 nchini, zinazokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kutokana na eneo hilo kukumbwa na ukame mkali.

 
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amebainisha kuwa, wilaya zaidi ya 45 nchini ziko hoi kwa ukosefu wa  chakula, sababu ikielezwa kuwa ni kukithiri kwa ukame.
Waziri huyo amewaonya wafanyabiashara kuwa na utu kwa kuacha kuwaumiza wananchi kwa kupandisha bei ya chakula.
Akihutubia wananchi katika vijiji mbalimbali vya Kata za Kwamsisi, Kwasunga na Kwaluguru, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Dk Kigoda alisema kuwa, wilaya hiyo ni miongoni mwa wilaya kati ya 45 nchini, zinazokabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, kutokana na eneo hilo kukumbwa na ukame mkali, hivyo kusababisha baadhi ya wakazi wake kula mboga za majani.
Kufuatia upungufu huo wa chakula, kumesababisha mfumko mkubwa wa bei ya mahindi na unga wa sembe kuwa juu, ambapo, Handeni gunia moja la kilo 100 za mahindi limefikia kuuzwa kati ya Sh90,000 hadi Sh100,000, kiwango ambacho hakijawahi kutokea wilayani humo.
Dk Kigoda ambaye pia ni Mbunge wa Handeni, alikutana na changamoto kubwa ya wananchi kumlilia chakula cha msaada ama kinachoweza kuuzwa kwa bei nafuu vijijini, wakidai wengi wao wanakula mlo mmoja kwa siku au kukosa kabisa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kwamsisi, Athumani Mwagahazi, alimweleza waziri huyo kuwa, wananchi wengi katika eneo hilo sasa wanaishi kwa kula maembe ya kuchemsha pamoja na majani ya mchunga.
Akizungumzia hali hiyo Dk Kigoda aliwaeleza wananchi hao kwamba, Serikali inatarajia kusambaza chakula kinachotarajiwa kuuzwa kati ya Sh700 hadi Sh850 kwa Mkoa wa Tanga, ambao unatarajiwa kuwafikia wananchi wiki hii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Hassan Mwachibuzi, alisema kwamba wanatarajia kupata tani 150 za unga wiki hii, utakaouzwa Sh750 na 900 kwa kilo moja vijijini katika Mkoa wa Tanga.

 Aina mbalimbali za vyakula
 
Mwachibuzi alisema bei hizo zinatofautiana kutokana na gharama za usafirishaji kutoka Jijini Dar es Salaam na maeneo ya mkoa huo, akisema kwa wilaya ya Handeni ambayo ndiyo iliyopo karibu na jiji hilo, kitauzwa na wafanyabiashara kwa bei ya Sh750.

No comments:

Post a Comment