Wednesday, January 2, 2013

ewura yashusha bei ya mafuta,kitendawili kilichobaki kwa wananchi ni kwamba JE NAULI NAZO ZITASHUKA? au ndio!!!!!!!!!!!!!

 
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imetangaza bei kikomo cha bidhaa za mafuta kinayoonyesha kuwa petroli, dizeli na mafuta ya taa zimeshuka kuanzia leo.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu imesema bei hizo zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Desemba 5, mwaka jana.
“Katika toleo hili, bei za rejareja kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, zimepungua kwa viwango vifuatavyo: petroli Sh126 kwa lita sawa na asilimia 5.96; dizeli Sh32 kwa lita sawa na asilimia 1.60 na mafuta ya taa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.50,” imeeleza taarifa hiyo.
Kwa punguzo hilo, bei ya rejareja ya petroli katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh1,993, dizeli Sh1,967 na mafuta ya taa Sh1,973. Arusha petroli ni Sh2,077, dizeli Sh2,051 na mafuta ya taa Sh2,057.
Katika jiji la Mbeya petroli itauzwa kwa Sh2,099, dizeli Sh2,074 na mafuta ya taa Sh2,079 na jijini Mwanza, petroli itauzwa kwa Sh2,142, dizeli Sh2,117 na mafuta ya taa Sh2,122.
Taarifa imefafanua kuwa mbali na kupungua bei hiyo katika uuzaji wa rejareja, bei pia imepungua kwa katika uuzaji wa jumla ikilinganishwa na matoleo mawili yaliyopita.
“Bei za jumla kwa kulinganisha matoleo haya mawili zimepungua kama ifuatavyo: petroli kwa Sh126.10 kwa lita sawa na asilimia 6.17; dizeli kwa Sh32.48 kwa lita sawa na asilimia 1.69 na mafuta ya taa kwa Sh50.74 kwa lita sawa na asilimia 2.6,” alisema.
Mkurugenzi huyo amesema katika taarifa hiyo kuwa mabadiliko hayo ya bei, yametokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kuimarika kidogo kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.
Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mafuta ya mwaka 2008, bei za bidhaa za mafuta ya petroli, zitaendelea kupangwa na soko.
“Ewura itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya uamuzi stahiki kuhusu ununuzi wa bidhaa za mafuta,” alisema Masebu.
Hata hivyo, Masebu alisema pamoja na mpango huo wa Ewura kuweka bei ya kikomo, kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa hizo kwa bei ya ushindani, ilimradi ziwe chini ya bei hiyo kikomo.
Alivitaka vituo vya mafuta kuchapisha bei hizo mpya katika mabango yanayoonekana bayana na kuonyesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta kutoka kwenye vituo vinavyouza mafuta kwa bei ndogo zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja na adhabu itatolewa kwa kituo husika,” alisema.
Masebu aliwashauri wanunuzi kuchukua stakabadhi ya malipo inayoonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita ili itumike baadaye kama kidhibiti endapo kutajitokeza malalamiko ya ama kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko ya kikomo au yenye kiwango cha ubora kisichofaa.


No comments:

Post a Comment