Tuesday, February 5, 2013

elimu yetu inavyojenga matabaka katika jamii.


 wanafunzi wa shule ya msingi wakiwa darasani,hii ndio tofauti kubwa kati ya shule yenye kutoa maarifa na ujuzi na shule yenye kutoa vyeti na sifa za kumuwezesha mtu kupata kazi.


MATOKEO mazuri au mabaya  ya elimu kwa mtu,  huonekana katika namna anavyotenda mambo na dhamira yake ya kutenda,  na wala hayatokani na alichojifunza, namna alivojifunza na sababu ya kujifunza.
Hiyo ndio tofauti kubwa kati ya shule yenye kutoa maarifa na ujuzi na shule yenye kutoa vyeti na sifa za kumuwezesha mtu kupata kazi.
Watu wengine wanapozungumzia elimu wanafikiri kuhusu utaratibu mzima wa kujifunza wenye lengo la kumpatia mtu ujuzi na maarifa na kumudu vyema kile alichojifunza.
Ujuzi na maaarifa ndio hasa lengo na upatikanaji wake  unaotarajiwa utumike katika kupambana na changamoto na hata kuibua na kuleta maarifa mengine zaidi.
Kuna watu wengine wanapozungumzia elimu,  wanafikiria umiliki wa cheti kinachoonyesha una ujuzi fulani.
Elimu ya aina hii sio kwa ajili ya kutumika katika maisha wala kutafuta maarifa mengine,  bali ni kwa ajili ya mtu kukariri anachojifunza na  kuyatoa yale maarifa yaliyokaririwa katika mitihani ili apate cheti kizuri kitakachowezesha kupata kazi yenye kipato kizuri.
Kimsingi,  cheti kazi yake ni kumpatia mtu kazi. Cheti ndio ‘pasipoti’ ya kwenda katika nchi ya kipato.
Watanzania wengi kama sio wote,  tumeangukia katika kundi hili. Wengi wetu tunataka pasipoti ya kwenda katika ‘nchi’ ya kipato cha kuajiriwa, tunataka vyeti!
Katika mfumo wetu wa elimu mpaka sasa ufaulu wa mtihani ndio unaosema fulani apangiwe shule gani, apangiwe kozi gani  chuoni, apate kiasi gani kwenye mikopo ya elimu ya juu na apangiwe kazi gani na alipwe kiasi gani.
Sasa kuna vita kati yetu, kila mmoja anataka mwanawe, yeye mwenyewe au ndugu yake  afaulu ili afike katika nchi ya ahadi.
Mbinu mbalimbali zinatumika  kufanikisha lengo hili, vita haina macho! Mbinu kuu ikiwa matumizi ya pesa. Kusoma shule nzuri na ghali, kulipia twisheni, walimu bora, kununua vitabu na mwishowe hata kununua mitihani.
Mchakamchaka  huu wa kutaka kufaulu kisha kupata vyeti,  unawaacha nyuma watu wa kipato cha chini kwani hawawezi kumudu kununua mitihani, au kusoma twisheni  za gharama.
Wenye nacho wananeemeka na mtindo huu. Mwelekeo unaonyesha masikini  wataachwa kwa kiasi kikubwa na wenye uwezo.
Mwanzo wa kujenga matabaka mawili kupitia elimu bila kificho  unaonekana.

No comments:

Post a Comment